TANZIA :MWANAHABARI FATUMA SHABAN IBRAHIM AFARIKI DUNIA
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imepokea kwa simanzi kubwa taarifa za kifo cha mtumishi wake mpendwa, Bi Fatuma Shaban Ibrahim, aliyekuwa Afisa Habari.
Marehemu alifariki dunia asubuhi ya tarehe 7 Julai 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, alipokuwa akiendelea kupata matibabu.
Taarifa hii imeacha pengo kubwa si tu kwa familia yake, bali pia kwa watumishi wenzake na jamii pana ya Ilemela.
Fatuma Shaban Ibrahim alitambulika kama mtumishi mwenye nidhamu, uadilifu na moyo wa kujitolea.
Katika nafasi yake ya Afisa Habari, alihakikisha kuwa taarifa za Halmashauri zinawafikia wananchi kwa uwazi na kwa wakati.
Alikuwa daraja muhimu kati ya uongozi wa Halmashauri na wananchi, akihakikisha sauti za wananchi zinasikika na changamoto zao zinawasilishwa kwa uongozi husika. Kupitia juhudi zake, alisaidia kuimarisha mawasiliano na kujenga imani ya wananchi kwa taasisi ya umma.
Zaidi ya majukumu yake ya kikazi, marehemu alijulikana kwa tabia yake ya upole na heshima kwa kila mtu. Alikuwa mfano wa kuigwa kwa watumishi wenzake, akionesha mshikamano na mshirikiano wa dhati. Wengi waliobahatika kufanya kazi naye wanamkumbuka kwa maneno yake ya faraja na tabasamu lake lililokuwa kioo cha matumaini hata katika nyakati ngumu.
Msiba huu umeacha majonzi makubwa kwa familia yake, ndugu, jamaa na marafiki.
Taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwao Tanga, ambapo familia na jamii nzima wanakusanyika kumpa heshima zake za mwisho.
Ni wakati wa mshikamano na maombi, tukimuomba Mwenyezi Mungu awape faraja wote walioguswa na msiba huu mzito.
