Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 SHEKHE AONYA CHUKI, ATAKA JAMII KUMRUDIA MUNGU

SHEKHE AONYA CHUKI, ATAKA JAMII KUMRUDIA MUNGU

NA MATUKIO DAIMA MEDIA

SINGIDA.‎Shekhe wa Mkoa wa Singida, Issah Nassoro, amewataka waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na viongozi wote wa kisiasa nchini, kujenga utamaduni wa kuheshimiana na kuepuka kauli za chuki zinazoweza kuwagawa na hata kuvuruga amani na mshikamano wa jamii.

‎Akihutubia mamia ya waumini katika swala ya Eid al-Adha iliyofanyika viwanja vya Bombadia mjini Singida, Shekhe alhaji Issah Nassoro alisema dini ya Kiislamu inahimiza upendo, heshima na mshikamano badala ya kukashifiana baina ya viongozi wa dini au wa kisiasa.

‎Alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakijenga uhasama usio na tija, jambo linaloongeza migawanyiko na chuki katika jamii, huku akihoji kama kweli bado wana hofu ya Mungu katika maisha yao ya kila siku.

‎Shekhe Nassoro alisema baadhi ya watu wamekuwa wakihofia zaidi umasikini kuliko hata kumcha Mungu, hali inayochangia kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili katika jamii.

‎Alieleza kuwa baadhi ya wanawake wamekuwa wakihofia kuingia kwenye ndoa na kuamua kuishi maisha ya “single mother”, huku baadhi ya wanaume nao wakijihusisha na vitendo visivyokubalika kijamii, jambo alilosema linapaswa kuwaamsha watu kurejea kwa Mwenyezi Mungu.

‎Aidha, aliwataka Waislamu wa Mkoa wa Singida kudumisha amani, kuwaheshimu viongozi wao wa dini, viongozi wa serikali pamoja na kuepuka uchonganishi unaoweza kuleta migogoro na chuki miongoni mwa viongozi na wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa Manispaa ya Singida, Abdalah Mkoko, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema Eid al-Adha ni siku ya upendo, mshikamano na kuwajali watu wenye mahitaji mbalimbali wakiwemo yatima, wagonjwa na wasiokuwa na uwezo.

‎Mkoko aliwataka pia Waislamu kuvumiliana, kusaidiana na kumaliza migogoro yao ya kidini, ili kujenga umoja, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi nao kuwalea vijana katika maadili mema, ili kuepuka vitendo vya ukahaba na mmomonyoko wa maadili kwa vijana.

Alisema amani ikitoweka hata ibada zitakuwa ngumu kufanyika kutokana na vurugu zinazoweza kujitokeza, huku akiihakikishia jamii kuwa serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kulinda na kuimarisha amani nchini.

‎Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Mirambo Camil Yusufu, aliyesali swala ya Eid al-Adha mkoani Singida, alisema maridhiano yaliyopendekezwa na Tume ya Jaji Chande ni muhimu kwa kurejesha umoja, upendo na mshikamano nchini, na akasisitiza kuwa Tanzania haiwezi kufikia maendeleo yaliyokusudiwa bila ya kuwepo kwa msamaha na maridhiano ya kweli.

‎Mirambo alisema katika vurugu za oktoba 29, 2026, baadhi ya wananchi wamepoteza maisha, wengine kujeruhiwa na kubaki na ulemavu, huku nazo mali za watu wengine zikiharibiwa kwenye matukio mbalimbali ya vurugu hizi, jambo alilosema linaonyesha umuhimu wa taifa kujenga utamaduni wa kusameheana na kutafuta suluhu badala ya chuki na visasi.

Alisema hata vitabu vitakatifu vya Quran na Biblia vinafundisha umuhimu wa maridhiano na kusameheana, akitolea mfano nchi ya Afrika Kusini, Rwanda na Burundi, ambazo zimefanikiwa kurejesha amani ya kweli, baada ya kuendekeza migogoro na chuki zisizokuwa na lazima miongoni mwa wananchi wake.

‎MWISHO

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3