SHEIKHE SHAABAN: UTII NA HESHIMA YA MAMLAKA NI MSINGI WA AMANI
WAUMINI wa dini ya Kiislamu wametakiwa kuendelea kuzingatia maadili ya usikivu, utiifu na kuheshimu viongozi pamoja na mamlaka halali ili kuimarisha amani na mshikamano katika jamii.
Wito huo umetolewa na Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu Shaaban, wakati wa ibada ya Eid El Hajj iliyofanyika katika Msikiti wa Gaddafi.
Amesema siku za Dhulhijjah zimebeba mafunzo muhimu ya utii na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, huku akiwahimiza Waislamu wenye uwezo kutekeleza ibada ya kuchinja kama sehemu ya kutimiza mafundisho ya dini.
Kwa mujibu wa Sheikhe Shaaban, simulizi ya Nabii Ibrahim na mwanawe Nabii Ismail ni somo kubwa linalofundisha jamii umuhimu wa kusikilizana, kuheshimiana na kutekeleza maagizo kwa uaminifu.
“Mafundisho haya yanatukumbusha umuhimu wa kuwa na nidhamu, kuheshimu mamlaka na kuishi kwa kusikilizana ndani ya jamii,” amesema.
Ameeleza kuwa ukosefu wa utiifu na usikivu mara nyingi husababisha migogoro, vurugu na kuvunjika kwa mshikamano wa kijamii, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kulinda amani kuanzia katika familia hadi ngazi ya Taifa.
Aidha, amesema dini ya Kiislamu inasisitiza kuwaheshimu viongozi wa dini, Serikali pamoja na taasisi mbalimbali zinazohusika na ustawi wa jamii.
Katika hatua nyingine, amewahimiza wananchi kuamini na kuheshimu mifumo pamoja na taasisi halali zinazoundwa kusimamia masuala ya kijamii na kidini ikiwemo BAKWATA.
Amesema kujenga utamaduni wa kuheshimu maamuzi ya viongozi na taasisi ni njia muhimu ya kudumisha utulivu, umoja na maendeleo ya Taifa.
Mwisho
.jpeg)

