SHEIKH KABEKE, MMOMONYOKO WA MAADILI UNAITIKISA JAMII, WAZAZI WATAKIWA KUSIMAMA KWENYE MALEZI.
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
MWANZA, Jamii imetakiwa kurejea katika misingi ya maadili, ibada na malezi bora ili kukabiliana na ongezeko la mmomonyoko wa maadili unaoendelea kujitokeza katika familia na jamii kwa ujumla.
Wito huo umetolewa Mei 27, 2026 na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke, wakati akitoa hutuba ya Sikukuu ya Eid Al Adha katika viwanja vya Nyamagana wilayani Nyamagana na kueleza kuwa hali hiyo imechangia baadhi ya watoto kuvunja heshima kwa wazazi na walezi wao, jambo ambalo linaashiria kuporomoka kwa maadili katika jamii.
Sheikh Kabeke amesema jamii ya leo imeendelea kukumbwa na ushawishi wa dunia na baadhi ya watu kufanya mambo yasiyokubalika bila kuzingatia mafundisho ya Mungu.
“Tunapaswa kuwatii wazazi na walezi, lakini pia wazazi wanapaswa kusimama imara katika suala la malezi. Anguko kubwa lililopo katika jamii yetu linatokana na mmomonyoko wa maadili,” amesema Sheikh Kabeke.
Aidha, amesema ipo haja ya familia kuimarisha ibada na mshikamano wa kifamilia ili kujenga kizazi chenye maadili mema na hofu ya Mungu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yasin Ally, amewataka waumini wa dini ya Kiislamu kuendeleza utamaduni wa ibada, utoaji wa sadaka na kulinda usalama wa watoto hasa katika kipindi cha sikukuu.
Yasin amesema mara nyingi watoto wanaoachwa kutembea peke yao wakati wa sikukuu hukumbana na hatari mbalimbali ikiwemo ushawishi wa vitendo viovu, ukatili na madhara mengine ya kijamii.
“Mzazi unayependa familia yako na umefanya maandalizi ya ibada na sadaka, ni muhimu kutowaacha watoto watoke peke yao bila uangalizi, kwani tumeshuhudia baadhi yao wakikumbana na vitendo vya kikatili,” amesema Yasin.
Naye Mwenyekiti wa JUWAKITA Mkoa wa Mwanza, Amina Masenza, amesema msingi wa familia bora hujengwa na namna wazazi wanavyowalea watoto wao katika misingi ya dini na maadili.
Amesema mfano wa utii na malezi bora unaonekana katika simulizi ya Nabii Ismail aliyeridhia maagizo ya Mwenyezi Mungu kupitia baba yake, hali inayoonesha umuhimu wa malezi sahihi kwa watoto.
Amina ametoa wito kwa jamii na familia kuhakikisha watoto wanalelewa kwa misingi ya dini ili kuwajengea uoga wa kutenda maovu na kuwafanya kuwa raia wenye maadili mema katika jamii.
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)