Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 MBEYA DC YAUNDA KAMATI KUTATUA KERO UTENGULE USONGWE.

MBEYA DC YAUNDA KAMATI KUTATUA KERO UTENGULE USONGWE.

 

NA JOSEA SINKALA, MBEYA DC.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Mhe. Aidda Haule, ameunda kamati za wajumbe watano katika kila Kitongoji kwenye Vitongoji vitatu vya Ihombe, Iwala na Idugumbi kata ya Utengule Usongwe wilayani Mbeya kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa mipango ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.

Hayo yamejiri wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi iliyofanyika katika Kata ya Utengule Usongwe.

Kamati hizo zitakuwa na jukumu la kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa maazimio na miradi mbalimbali inayolenga kutatua changamoto zilizobainishwa na wananchi katika maeneo yao.

Kupitia mfumo huo, kila Kitongoji kitaweka alama ya “vema” kwa maeneo yaliyotekelezwa kwa mafanikio na alama ya “mkasi” kwa yale ambayo hayajatekelezwa ili kurahisisha ufuatiliaji na uwajibikaji katika kufikia maendeleo endelevu.

Akizungumza na wananchi katika ziara hiyo, Mhe. Aidda Haule amesema kamati hizo zitakuwa na mamlaka ya kuongeza changamoto nyingine katika orodha ya maeneo ya utekelezaji kulingana na mahitaji ya Kitongoji husika kwa ajili ya kufikishwa kwenye mamlaka zinazohusika, hatua inayolenga kuhakikisha sauti za wananchi zinaendelea kusikika na changamoto zao kutatuliwa kwa ukaribu na hatimaye kupatiwa ufumbuzi.


Mhe. Aidda Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya na Diwani wa kata hiyo amewahakikishia wananchi kuwa Halmashauri itaendelea kushirikiana nao katika kutatua changamoto mbalimbali na kusimamia maendeleo ya maeneo yao.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3