Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SERIKALI YAJIVUNIA MAFANIKIO YA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

SERIKALI YAJIVUNIA MAFANIKIO YA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Dodoma

SERIKALI imesema hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya zimeanza kuzaa matunda baada ya kiwango cha bangi kinachokamatwa nchini kupungua kwa kiasi kikubwa mwaka 2025.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya dawa za kulevya nchini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema operesheni zilizofanywa na vyombo vya usalama zimechangia kudhibiti usambazaji wa dawa hizo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tani 1,017.26 za bangi zilikamatwa mwaka huu, huku kiwango hicho kikionyesha upungufu wa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka uliopita. 

" Mafanikio hayo yanatokana na kuimarishwa kwa operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi pamoja na kuongezeka kwa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya, " Amesema.

Prof. Kabudi alisema licha ya kupungua kwa bangi, bado dawa hiyo ndiyo inayoongoza kwa kukamatwa nchini kutokana na kuendelea kuwepo kwa mitandao ya biashara hiyo katika baadhi ya maeneo.

Katika hatua nyingine, amesema kuwa tani 26.36 za mirungi zilikamatwa mwaka huu, kiwango kilichoonyesha ongezeko ikilinganishwa na mwaka 2024. Serikali imesema ongezeko hilo linaonyesha kuimarika kwa doria na ukaguzi katika maeneo ya mipakani.

Taarifa hiyo pia imebainisha kukamatwa kwa dawa nyingine za kulevya za viwandani ikiwemo methamphetamine, heroin, cocaine pamoja na dawa aina ya MDMA na MDA.

Aidha, kwa mara ya kwanza nchini, mamlaka zilifanikiwa kukamata tani 29.52 za dawa mpya ya kulevya aina ya Kratom iliyokuwa imeingizwa nchini kwa njia ya udanganyifu ikielezwa kuwa ni mbolea.

Serikali pia ilitaifisha mali zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.3 zilizobainika kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya, huku mashauri zaidi ya elfu moja yakifunguliwa mahakamani dhidi ya watuhumiwa mbalimbali.

Mbali na operesheni za ukamataji, Waziri amesema inaendelea kutoa huduma za matibabu na ushauri kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ambapo zaidi ya watu 85,000 walipatiwa huduma hizo katika vituo tofauti nchini.

Prof. Kabudi alionya kuwa matumizi ya dawa za kulevya yanaendelea kuhatarisha ustawi wa jamii hasa kwa vijana, akieleza kuwa tatizo hilo linachangia ongezeko la vitendo vya uhalifu, migogoro ya kifamilia na kupotea kwa nguvu kazi ya taifa.

Amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kufichua mitandao ya biashara ya dawa za kulevya ili kulinda usalama wa jamii na taifa kwa ujumla.

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3