SERIKALI YAAGIZA UDHIBITI MKALI WA MBEGU FEKI MIPAKANI KULINDA WAKULIMA,KUIMARISHA USALAMA WA CHAKULA
Na Hamida Ramadhan Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI imeendelea kusisitiza udhibiti mkali wa mbegu zinazoingia nchini kupitia mipaka, ikieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kulinda wakulima dhidi ya matumizi ya bidhaa zisizo na viwango na kupunguza malalamiko yanayoelekezwa kwa serikali.
Akizungumza wakati wa kufungua Mkutano wa Taifa wa Wadau wa Tasnia ya Mbegu 2026, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema ni lazima mamlaka za mikoa na wilaya za mipakani ziimarishe ukaguzi wa mara kwa mara wa mbegu ili kuhakikisha zinazoingia nchini zinakidhi viwango vilivyowekwa.
Silinde amesema baadhi ya mbegu zimekuwa zikipita mipakani bila kufanyiwa tathmini ya kutosha jambo linalosababisha hasara kubwa kwa wakulima na kuathiri uzalishaji wa mazao nchini.Aidha, ametoa wito kwa Jeshi la Magereza kuongeza jitihada katika uzalishaji wa mbegu bora zinazostahimili ukame pamoja na mbegu za mazao ya kimkakati ili kusaidia kupunguza uhaba wa mbegu nchini.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kampuni za mbegu nchini kuelekeza nguvu katika kuzalisha mbegu zinazoweza kustahimili mabadiliko ya tabianchi na magonjwa ya mimea ili kuongeza tija kwa wakulima na kukuza viwanda vya ndani.
Kwa upande wa sekta ya fedha, Silinde ameitaka taasisi za kifedha kubuni mikopo yenye masharti nafuu itakayowawezesha wazalishaji wa mbegu na wakulima kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kilimo.
Amesema maendeleo ya sekta ya mbegu yanahitaji mtaji mkubwa, hususan katika miundombinu ya umwagiliaji na vifaa vya kuchakata mazao baada ya mavuno.
Katika hatua nyingine, ameitaka serikali za mitaa kuhakikisha zinatenga maeneo maalum kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu ili kuongeza upatikanaji wake nchini, akisisitiza kuwa uratibu huo ni muhimu katika kufanikisha malengo ya kilimo cha kisasa.
"Wilaya ya Tanganyika imekuwa mfano kwa kutenga eneo kubwa la ardhi kwa ajili ya shughuli za uzalishaji wa mbegu, hatua inayotarajiwa kuigwa na maeneo mengine, " Amesema.
Aidha, ameitaka sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha tafiti, kujenga uwezo wa taasisi na kuboresha mifumo ya uzalishaji wa mbegu nchini.
"Takwimu zilizotolewa katika mkutano huo zinaonyesha kuwa matumizi ya mbegu bora bado yako chini, huku changamoto ya uzalishaji wa ndani na gharama za mbegu ikiendelea kuathiri wakulima wengi, " Amesema
Mkurugenzi Mtendaji wa ASPIRES Tanzania, David Nyange amesema uzalishaji mdogo wa kilimo ni kikwazo kikubwa kwa usalama wa chakula, akisisitiza haja ya kuongeza upatikanaji na matumizi ya mbegu bora nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Justina Rahi amesema bado kuna pengo kubwa kati ya mahitaji na uzalishaji wa mbegu nchini, hali inayohitaji hatua za haraka za kimkakati.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uthibitishaji Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha ubora wa mbegu unazingatiwa sambamba na kufanikisha malengo ya muda mrefu ya sekta ya kilimo nchini.


.jpeg)
.jpeg)