HAIPPA YAZINDUA KAMPENI YA ELIMU YA ELIMU YA UWEKEZAJI KWA WATANZANIA.
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
MWANZA, Kampuni ya uwekezaji na ukuzaji biashara Tanzania, Haippa PLC, imezindua Jukwaa la Taifa la Tanzania Tuwekeze pamoja na kampeni maalum ya kutoa elimu ya uwekezaji kwa Watanzania ili kuongeza uelewa kuhusu ushiriki wa wananchi katika uchumi na uwekezaji wa makampuni makubwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Haippa, Boniphace Ndengo, amesema jukwaa hilo linalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu dhana ya uwekezaji, hisa, hati fungani pamoja na namna ya kutumia mitaji midogo kushiriki katika uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Ndengo amesema kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya wananchi wanaojishughulisha na ujasiriamali mdogo katika sekta zisizo rasmi, hivyo kuna umuhimu wa kuwaunganisha katika mfumo rasmi wa uchumi ili waweze kunufaika zaidi na fursa za uwekezaji.
“Jukwaa hili ni kampeni mahsusi ya kuwasaidia Watanzania kuelewa kuwa hata wenye mitaji midogo wanaweza kushiriki kwenye umiliki wa makampuni makubwa na kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wa taifa,” amesema Ndengo.
Mbali na elimu ya uwekezaji, amesema jukwaa hilo pia litazindua kampeni ya kukuza ubunifu nchini kwa kushirikiana na vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za elimu, kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kutumia maarifa yao kuanzisha biashara na kutengeneza ajira.
“Dunia ya leo imejengwa kupitia ubunifu na teknolojia, lakini mara nyingi taasisi za elimu zimekuwa zikizalisha vijana wanaotoka kwenda kutafuta ajira. Kupitia programu hii tunataka kushirikiana na vyuo vikuu kujenga kizazi cha wabunifu na waajiri,” amesema Ndengo.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inaunga mkono maono ya serikali ya kujenga uchumi mkubwa unaolenga kufikia uchumi wa dola trilioni moja katika miaka ijayo.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Kanda wa TISEZA, Phina Jerome, amesema Jukwaa la Tanzania Tuwekeze limeanzishwa ili kuunganisha serikali, sekta binafsi, wawekezaji pamoja na wadau wa maendeleo katika kujadili na kuonesha fursa zilizopo nchini hususani katika Kanda ya Ziwa.
Phina amesema Kanda ya Ziwa ina utajiri mkubwa wa rasilimali, utalii na fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali, huku serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia huduma rahisi za uwekezaji, vivutio vya kiuwekezaji na uratibu wa maeneo maalum ya kiuchumi.
Amesema jukwaa hilo litasaidia kuongeza uwekezaji, kuvutia mitaji na teknolojia, kujenga mitandao ya biashara pamoja na kuongeza ajira na thamani ya mazao ya ndani.
Aidha, amesema kupitia jukwaa hilo kumekuwa na ongezeko la ushiriki wa vijana, wanawake, wajasiriamali na wabunifu katika miradi ya uwekezaji, hali inayotarajiwa kuleta manufaa kwa wananchi na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kinene, amesema vijana ni nguvu kazi kubwa inayohitaji fursa mbalimbali za kiuchumi kupitia uwekezaji, biashara, ajira na elimu ili kujikwamua kiuchumi.
Kinene amesema kupitia majukwaa ya uwekezaji kama HAIPPA, vijana wengi wanatarajiwa kupata maarifa na mbinu zitakazowawezesha kufikia mitaji na kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za uchumi.
Amesema kuna aina tatu za msingi za uwekezaji ambazo ni uwekezaji kupitia ajira, biashara pamoja na elimu, huku akieleza kuwa Mkoa wa Mwanza una nafasi kubwa ya kuvutia wawekezaji kutokana na jiografia yake na wingi wa fursa zilizopo.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nyihita Sunflower kilichopo Wilaya ya Rorya Mkoani Mara, Nyihita Nyihita, amesema aliamua kupeleka ubunifu wake kijijini kwa kuanzisha kiwanda cha kuchakata mafuta ya alizeti ili kusogeza maendeleo karibu na wananchi.
Nyihita amesema tofauti na mtazamo wa wengi wanaoamini viwanda vinapaswa kujengwa mijini pekee, yeye aliona umuhimu wa kupeleka uwekezaji vijijini ili kutoa fursa kwa wananchi wa kawaida.
“Nilianzisha kiwanda kijijini ili kupeleka ubunifu na fursa kwa wananchi wa kawaida kutokana na viwanda vingi kuwa mjini. Ubunifu huu umeleta matokeo chanya kwa kuwahamasisha wananchi kulima alizeti, kupata kipato na kuwainua vijana wajasiriamali wanaochukua mafuta kiwandani na kwenda kuuza,” amesema Nyihita.
Hata hivyo, amesema mwanzo wa mradi huo ulikumbwa na changamoto za wananchi kutokuwa na imani kuwa kiwanda kinaweza kujengwa kijijini, hali iliyowafanya baadhi yao kudhani jambo hilo haliwezekani.
“Waliamini viwanda vinajengwa mjini na si vijijini, hivyo wengi walishangaa na kujiuliza nitapataje malighafi huku kijijini,” amesema.
Kwa mujibu wa Nyihita, kuanzishwa kwa kiwanda hicho kumechangia utoaji wa ajira kwa vijana na wakulima zaidi ya 3,020, huku kiwanda kikizalisha takribani tani 8,600 za bidhaa kwa siku.
.jpeg)

.jpeg)
