NSOMBA ASISITIZA UMOJA NA USHIRIKIANO CCM MBEYA MJINI.
Na Samwel Mpogole: Mbeya.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini, Afrey Nsomba amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kuendelea kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano ili kuleta maendeleo ndani ya chama na kwa wananchi kwa ujumla.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya, Nsomba amesema ni muhimu kwa viongozi na wanachama kuacha makundi na kufanya kazi kwa pamoja kwa kuwa wote wanabeba dhamana ya kukijenga chama hicho.
Aidha amesema viongozi wanapaswa kuwa imara na kupambana katika kutekeleza majukumu yao badala ya kuwa wanyonge na kushindwa kutumia nafasi walizopewa kwa maendeleo ya chama na wananchi.
Pia Mwenyekiti huyo amesema anatarajia kufanya ziara katika kata mbalimbali za Wilaya ya Mbeya Mjini kwa lengo la kuimarisha chama na kusikiliza changamoto zinazowakabili wanachama pamoja na wananchi.
Amesema mafanikio ya ziara hiyo yatategemea ushirikiano kutoka kwa viongozi wa chama ngazi zote pamoja na wanachama kwa ujumla.
Sambamba na hilo, Nsomba amesema wanatarajia kuanzisha Jogging Club ya CCM Mbeya Mjini ambayo itakuwa na lengo la kuimarisha afya, umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi na wanachama wa chama hicho.
Amefafanua kuwa klabu hiyo itakuwa ikifanya mazoezi ya jogging kila Jumamosi huku ikitarajiwa kuwa sehemu ya kuwaunganisha wanachama pamoja na kuhamasisha afya bora kwa jamii.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao hicho wameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha chama kinaendelea kuwa imara na kutimiza malengo yake ya maendeleo kwa wananchi.
MWISHO.

.jpeg)
.jpeg)
