MISAADA YAENDELEA KUWAFIKIA WAATHIRIKA WA MAFURIKO MOVEMERO
Na Matukio Daima, Mvomero
Misaada ya chakula, magodoro na mahitaji mbalimbali ya kibinadamu imeendelea kuwafikia waathirika wa mafuriko katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, huku jamii hiyo ikiendelea kuiomba Serikali kuwapatia makazi ya kudumu pamoja na maeneo ya kilimo ili waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida.
Shirika la Compassion International Tanzania kwa kushirikiana na makanisa ya EAGT MANYINGA na FPCT TURIANI wamefika katika makambi ya waathirika hao na kutoa msaada huo, huku likipanga pia kujenga nyumba 15 kwa baadhi ya familia zilizoathirika zaidi
Baadhi ya waathirika akiwemo Elizabeh Mbagga na Aisha Amin wamesema maisha yao yamekuwa magumu baada ya mafuriko kuharibu nyumba na mali zao, na sasa wanaendelea kuishi kambini wakisubiri suluhisho la kudumu la makazi na ardhi ya kilimo.
Akisoma Risala wakati wa makabidhiano hayo
Usia Evod kutoka kituo cha huduma ya mtoto na kijana kanisa la FPCT Turiani amesema wameguswa kutoa msaada hiyo ili kupunguza magumu wanayokabiliana nayo waathirika hao wa mafuriko.
Meneja wa Compassion Kanda ya Mashariki, Shiphrah Mwagisa, amesema shirika hilo litaendelea kusaidia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha waathirika wanapata huduma muhimu na makazi ya muda na ya kudumu.
Amesema msaada wa chakula, magodoro na mahitaji mengine waliotoa una thamani ya Shilingi milioni 8.43 na kwamba awali shirika hilo pia lilitoa msaada mwingine uliogharimu shilingi milioni 8.64 awali pamoja na kuwakodishia nyumba kwa muda wa miezi sita baadhi ya waathirika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Maulid Dotto, licha ya kushukuru kwa msaada huo, amesema Serikali inaendelea na mipango ya kutafuta maeneo salama na kuhakikisha mto unarudishwa katika mkondo wake wa asili ili kupunguza madhara ya mara kwa mara.










