JKT YAWAITA VIJANA WALIOHITIMU KIDATO CHA SITA 2026 KURIPOTI MAKAMBINI KWA MAFUNZO YA LAZIMA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limewataka rasmi vijana wote waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita mwaka 2026 kutoka shule zote za Tanzania Bara na Zanzibar kuripoti katika makambi mbalimbali ya jeshi hilo kuanzia Juni 1 hadi Juni 7, 2026 kwa ajili ya kuanza mafunzo ya lazima kwa mujibu wa sheria za nchi.
Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi Mei 28, 2026 na Mkuu wa Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabene alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele.
Brigedia Jenerali Mabene amesema vijana wote waliochaguliwa wanapaswa kufika katika makambi waliopangiwa ndani ya muda uliotolewa ili kuanza mafunzo hayo yanayolenga kuwajengea uzalendo, nidhamu, utii, umoja wa kitaifa pamoja na stadi mbalimbali za maisha zitakazowasaidia katika mustakabali wao.
Amesema JKT tayari limekamilisha upangaji wa makambi kwa wahitimu hao ambapo baadhi ya makambi yatakayopokea vijana ni pamoja na Rwamkoma, Msange, Ruvu JKT, Mpwapwa, Makutupora, Mafinga, Male, Mgambo, Maramba, Makuyuni JKT, Oljoro, Bulombora, Kanembwa, Mtabila, Itaka, Luwa, Milundikwa pamoja na Nachingwea.
Makambi mengine yaliyotajwa ni pamoja na Chuo cha Uongozi JKT (CUJKT) kilichopo Kibiji jijini Dar es Salaam.
Aidha, Brigedia Jenerali Mabene amesema wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho wanatakiwa kuripoti katika kambi ya Ruvu JKT ambayo ina miundombinu rafiki kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye mahitaji maalum.
Kuhusu vifaa muhimu vya kwenda navyo kambini, vijana wametakiwa kuwa na kaputura ya rangi ya dark blue yenye elastic kiunoni isiyo na mfuko wa nyuma na yenye urefu wa kufika magotini, fulana ya kijani, raba za michezo za rangi ya kijani au blue, shuka mbili za blue bahari pamoja na soksi nyeusi.
Pia wale waliopangiwa makambi yenye hali ya hewa ya baridi wametakiwa kuwa na mavazi ya kujikinga na baridi huku nyaraka zote muhimu zinazohitajika katika udahili wa elimu ya juu zikitakiwa kubebwa, ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya kuhitimu kidato cha nne pamoja na nyaraka nyingine muhimu za masomo.
Brigedia Jenerali Mabene amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla kwani mbali na kuwajengea uzalendo na nidhamu, pia huwapa ujuzi mbalimbali wa maisha na kujitegemea.
Amesisitiza kuwa si kila mhitimu ataendelea na elimu ya juu moja kwa moja, hivyo mafunzo ya JKT yatasaidia kuwajengea uwezo vijana watakaobaki katika jamii ili waweze kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.
Mwisho
