TRA YATOA ONYO KALI DHIDI YA MAGENDO TANGA, YAHIMIZA MATUMIZI YA BANDARI.
NA AMINA SAID,TANGA.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na uingizaji wa bidhaa nchini kwa njia za magendo, ikibainisha kuwa vitendo hivyo ni tishio kwa usalama wa taifa na afya ya jamii.
Meneja wa TRA mkoani Tanga amesema kuwa bidhaa za magendo siyo tu zinaikosesha Serikali mapato yanayostahili, bali ni hatari kwa afya ya mlaji,
Alifafanua kuwa bidhaa hizo hazipiti katika taasisi za udhibiti wa ubora, hivyo kuingizwa sokoni bila kuthibitishwa usalama wake.
Katika hatua nyingine, Meneja huyo alibainisha kuwa operesheni dhidi ya magendo zinaendelea nchi nzima na tayari wafanyabiashara kadhaa wameshakamatwa na kutozwa faini kubwa (Penalties). Alisisitiza kuwa, kwa mujibu wa sheria, chombo chochote kitakachokutwa kimebeba bidhaa za magendo kitataifishwa na Serikali kulingana na sheria.
Alisema pia kuhusu ukusanyaji wa mapato, Mamlaka imewataka wananchi kujenga utamaduni wa kudai risiti za kielektroniki (EFD) na kuwataka wafanyabiashara kutoa risiti halali kwa kila manunuzi.
Aidha amewahimiza wafanyabiashara kutumia Bandari ya Tanga, akisema kuwa hivi sasa inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kutoa mizigo kwa wakati, jambo linalochochea ukuaji wa biashara mkoani humo.
Kwa upande wa wafanyabiashara wenye madeni makubwa ya kodi, TRA imewashauri kufika ofisini kwa ajili ya majadiliano (Negotiations) ili kuwekewa utaratibu rafiki wa kulipa kodi hizo kwa awamu.
Mamlaka imeweka wazi uwepo wa "Dawati la Wafanyabiashara" ambalo jukumu lake kuu ni kutoa elimu na kusaidia kukuza biashara ndogo ziweze kufikia hatua ya kuwa walipakodi wakubwa.
Mwishoni mwa maelezo yake, Meneja huyo ametoa wito kwa wafanyabiashara wote kujitokeza kukadiriwa mapato yao mapema, Hatua hiyo inalenga kuepusha changamoto na usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa zoezi la ukaguzi wa bidhaa barabarani.

