Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YATOA MAFUNZO KWA WAJUMBE WA BODI ZA USULUHISHI WA NDOA

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YATOA MAFUNZO KWA WAJUMBE WA BODI ZA USULUHISHI WA NDOA



Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera 

Wizara ya Katiba na sheria imeanza kutoa mafunzo kwa wajumbe wa bodi za usuluhishi wa ndoa kwa mkoa wa Kagera lengo likiwa ni kuwaongezea uwezo wajumbe hao jinsi ya kutatua migogoro ya ndoa ili kuleta ustawi wa familia katika jamii.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Naibu katibu mkuu wa wizara hiyo Fraklin Rwezimula amesema kuwa kesi za talaka ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika kituo jumuishi cha utoaji haki takwimu zinaonyesha kuwa talaka 711 zilisajiliwa mwaka 2023, zikapanda hadi 1,569 mwaka 2024 na kufikia 1,172 mwaka 2025.

“hali hii ni mbaya zaidi katika jamii kwani idadi ya ndoa zinazovunjika bila kutolewa taarifa zinaongezeka hii inashiria uwepo wa changamoto katika usuluhishi wa migogoro ya ndoa kwenye jamii”

Kwa upande wake mkurugenzi wa huduma za sheria kwa umma kutoka wizara ya Katiba na sheria Obadia Mugasa amesema kuwa mafunzo hayo yanalengo wa kuwajengea uwezo wasuluhishi wa migogoro ya ndoa katika jamii na kujenga ustawi wa familia kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.


“mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo na mbinu wajumbe hawa za usuluhishi wa migogoro hii ukizingatia wakati na aina ya migogoro iliyopo kwa sasa hatua hii itasababisha wasuluhishi wetu kuwa na uwelewa wa kutosha  kushughulikia masuala haya kwa wakati”

Naye Kaimu katibu tawala mkoa wa Kagera Isaya Tendega amesema kuwa  migogoro ya ndoa ikiwa haitatuliwa katika bodi za usuruhishi wa migogoro ya ndoa inaongeza mzigo mkubwa kwa wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa.


“tumekuwa tukipokea kwa wingi migogoro ya ndoa katika ofisi zetu kwahiyo mafunzo haya kwa wajumbe wa bodi za usuluhishi wa ndoa itasaidia migogoro hii kutatuliwa kwa wakati na kupunguza mzigo kwa wakuu wilaya na mikoa”

Mmoja wa wajumbe wa bodi hizo Dakta Ruta Bachubila amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yanaenda kuwaelimisha wajumbe hao na itawajengea uwezo wa kusuluhisha migogoro hivyo kudumisha familia.


“mafunzo haya ni mazuri zaidi kuelimisha watu mpaka chini sio kuelimisha baraza tu waelimishe mpaka jamii iliyopo chini na itatujengea uwezo wa kusuluhisha na sio kuamua hivyo kudumisha familia na kuimarisha ndoa”

Mafunzo hayo ambayo yameanzia mkoani Kagera yatafanyika kwa siku tatu mkoani hapo, lengo likiwa ni kupunguza migogoro ya ndoa katika jamii.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3