SAME UTALII FESTIVAL FURSA KWA WANANCHI WILAYANI SAME
WANANCHI wilayani Same mkoani Kilimanjaro wamewaomba viongozi wilayani humo kuhakikisha tamasha la Utalii la Same festival kufanyika kila mwaka kwani linawasaidia kukuza uchumi wao.
Kauli hiyo ilitolewa leo na wakinamama lishe wilayani humo katika joggin ya kumahamasisha tukio hilo linalotarajiwa kufanyika Aprili 10 hadi 12 mwaka huu likiwa ni msimu wa tatu tangu kuanzishwa kwake.
Anna Mzava ambaye ni mama lishe katika stendi ya mabasi wilayani Same alisema kuwa, mbali ya tamasha hilo kuhamasisha Utalii lakini wao kama mama lishe wamekuwa wakijipatia kipato kutokana na wananchi kutoka maeneo mbalimbali kushiriki.
"Tunaomba hili tamasha liwe ni endelevu kwani sisi wananchi wa chini tunafaidika nalo biashara zetu zinaenda vizuri na tunapata fedha nyingi kama mimi badala ya kupika mchele kilo 3 siku ya tamasha napika kilo 10 na zinaisha zote" Alisema Anna.
Naye Jumanne Idd alisema kuwa, tamasha hilo limekuwa likichangia kutangaza Utalii unaopatikana wilayani humo pamoja na vyakula vya asili vya kabila la wapere ambapo limesaidia kuitangaza wilaya hiyo kitaifa.
Alisema kuwa, kupitia tukio hilo biashara nyingi zimekuwa zikichangamka msimu wa tukio hali ambayo inapelekea wananchi kupata vipato na kunufaika kiuchumi.
Akizungumza katika Joggin hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Same, Yusto Mapande alisema kuwa, wamejipanga kuhakikisha tamasha hilo linakuwa endelevu ambapo lengo lake ni kuhakikisha wanaendelea kutangaza vivutio vyote vya Utalii vilivyopo same.
Mapande alisema kuwa, wataendelea kuibua vivutio vipya na kuvitangaza viweze kujulikana na kuinua uchumi wa wananchi wilayani Same.
"Faida kubwa ambazo tunazitegemea kwa wananchi wa Same kupitia tamasha hili ni faida za kiuchumi kwani panapokusanyika watu wengi ni fursa kwani watahitaji huduma mbalimbali ambapo watazilipia huduma hizo" Alisema Mapande.

