MAREKANI YAKATAA MASHARTI YA IRAN
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Serikali ya Marekani imekataa rasmi mpango wa pointi 10 wa kusitisha mapigano uliotolewa na Iran, ikidai kuwa masharti hayo ni tofauti na yale yaliyokubaliwa na Ikulu ya Marekani (White House).
Marekani imebainisha kuwa Iran imeweka madai makubwa ambayo hayawezi kutekelezeka kwa sasa, jambo linalozidisha mvutano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Mvutano mkubwa unatokana na madai ya Iran kutaka kuendelea kurutubisha madini ya nyuklia na kutaka majeshi ya Marekani yaondoke Mashariki ya Kati.
Serikali ya Rais Donald Trump imesisitiza msimamo wa "Zero Enrichment" (kutovumilia nyuklia) huku Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, akitangaza wazi kuwa wanajeshi wa Marekani hawataondoka eneo hilo.
Pande hizo zinatofautiana kuhusu udhibiti wa Mlango wa Bahari wa Hormuz na ushiriki wa kundi la Hezbollah kwenye makubaliano hayo.
Wakati Iran ikitaka udhibiti kamili wa njia hiyo ya mafuta, Marekani inataka ibaki wazi kwa biashara ya dunia, huku ikisisitiza kuwa vita vya Lebanon ni suala tofauti na halipaswi kuingizwa kwenye mkataba huu.
Licha ya malumbano hayo, milango ya amani bado ipo wazi ambapo mazungumzo ya ana kwa ana yanatarajiwa kuanza rasmi Ijumaa hii, Aprili 10, 2026, jijini Islamabad, Pakistan.
Mazungumzo hayo yanalenga kuziba pengo la kimitazamo na kutafuta suluhu ya kudumu itakayomaliza mapigano na kurejesha utulivu katika ukanda huo wa Mashariki ya Kati.
