MWENYE ULEMAVU MPOKI AWAANGUKIA DKT. TULIA BAADA YA KUPOKEA KITI MWENDO NA MTAJI
Na Matukio Daima, Habari
Mbeya
MWENYE ulemavu Mpoki Abraham (33), mkazi wa mtaa wa Bombambili kata ya Mwakibete Jimbo la Uyole, amemshukuru Dkt. Tulia Ackson, Mbunge wa Jimbo la Uyole, kwa kumkabidhi kiti mwendo na mtaji wa sh. 500,000. Mpoki, ambaye ni mlemavu wa miguu na mikono, anataka kuwa mfanyabiashara mkubwa na anamwomba Dkt. Tulia kumwongozea nguvu ya mtaji mkubwa.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mpoki alisema kuwa Dkt. Tulia amekuwa mtu pekee aliyemwamini na kumsaidia. "Hapa Dkt.Tulia amenipatia msaada wa kiti mwendo na mtaji, naomba pia aendelee kunisapoti maana natamani kuwa mfanyabiashara mkubwa sana na Mungu atambariki sana maana hata huu mtaji wa sh.500,000 alionipatia mkubwa sana kwangu sikutegemea maana hapa nyumbani wamekuwa wakija watu wengi kuniahidi kunisaidia lakini huwa hawarudi lakini Dkt.Tulia amekuwa mtu pekee na wa utofauti kwangu," alisema Mpoki.
Lugano Mwangosi, Kiongozi wa mbio za Bendera ya Upendo ya Taasisi ya Tulia Trust, alisema kuwa Mpoki amekabidhiwa kiti mwendo na mtaji ili kumwinua kiuchumi.
"Ndugu yetu pia tumemkabidhi mtaji wa sh.500,000 ili kuweza kumwinua kiuchumi, tunahitaji Mpoki akue katika biashara yake hii ili tukija awamu nyingine awe amekua kibiashara zaidi ya hapa na tutaweza kumwinua tena ndugu yetu kwani hapa pia tumempatia kiti mwendo ambacho sasa kitarahisisha shughuli zake," alisema Mwangosi.
Hafla ya kukabidhi msaada huo ilifanyika April 2, 2026, ambapo Dkt. Tulia Ackson, Mbunge wa Jimbo la Uyole na Mkurugenzi wa Taasisi ya Tulia Trust, alitoa maelekezo kuwa wahitaji wote ambao walifikiwa na bendera wote wafikiwe na maenye ulemavu Mpoki amekuwa mtu wa kwanza kukabidhiwa kiti mwendo na mtaji.

