MILIONI 45 KUKOMESHA ADHA YA KINA MAMA KUJIFUNGULIA NJIANI
NA AMINA SAIDI, TANGA.
Wananchi wa Kijiji cha Kibaya, Wilayani Handeni, wapo ukingoni mwa kuondokana na kero ya muda mrefu ya huduma za afya baada ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa Shilingi Milioni 45.7 kwa ajili ya kukamilisha zahanati ya kijiji hicho.
Hatua hiyo inakuja kama ukombozi wa kijamii, ikilenga kuhakikisha miundombinu ya afya inamfikia mwananchi wa kawaida na kuimarisha hali ya matibabu katika maeneo ya pembezoni mwa Mkoa wa Tanga.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurahman Abdallah, amesema ufadhili huo unalenga kuimarisha miundombinu ya afya ili imfaidike mwananchi wa kawaida.
Alisisitiza kuwa kukamilika kwa zahanati hiyo kutapunguza changamoto za afya ambazo zimekuwa zikiwakabili wakazi wa eneo hilo kwa muda mrefu.
Aidha, Mwenyekiti huyo alitumia wasaa wa ziara yake kusikiliza kero mbalimbali za wananchi, ikiwemo ukosefu wa maji pamoja na ubovu wa barabara.
Alibainisha kuwa Rais Samia tayari ametoa Shilingi Bilioni 171 kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji mkoani humo, huku akiahidi kuwa serikali inafanyia kazi maboresho ya miundombinu ya barabara, hususan katika eneo la Mkata.
Katika hali ya kutia moyo, Mwenyekiti Rajabu amewaahidi wananchi wa Kibaya kuwa atahakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unakamilika bila kukwama.
Alikumbusha kuwa mradi huo ulianza baada ya wananchi kumsimamisha wakati wa ziara yake ya mwaka 2024 na kumwonyesha eneo walilotenga, ambapo yeye binafsi alichangia Shilingi Milioni 10 ili kuanza ujenzi.
"Iwe mvua ama jua, usiku au mchana, zahanati hii itakamilika ili kuondoa adha ya akina mama kujifungulia njiani," alisisitiza Rajab.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Steven Saitoti, amethibitisha kuwa serikali imeshachochea kasi ya mradi huo kwa kutoa Shilingi Milioni 45.7. Aliongeza kuwa kutokana na kasi ya ujenzi inayoendelea, mradi huo unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo mwanzoni mwa mwezi wa tisa mwaka huu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, ameeleza kuwa wilaya inashirikiana kwa karibu na wadau wa CCM na serikali kuhakikisha jengo hilo linakamilika kwa wakati.
Alisema nguvu za pamoja kati ya wananchi na viongozi ndizo zitakazowakomboa wananchi kutoka kwenye adha ya kufuata huduma za afya maeneo ya mbali.
Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kibaya wameeleza furaha yao na kumshukuru Rais Samia pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa kwa kuwasikiliza kilio chao.
Mmoja wa wakazi hao, Mwanahawa Athumani, amesema kukamilika kwa zahanati hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wanawake, kwani sasa watakuwa na uhakika wa usalama wao na watoto wao wakati wa uzazi bila hofu ya umbali.
Ziara hii ya Mwenyekiti Rajab ni sehemu ya mkakati wake wa kuimarisha Chama mkoani Tanga, ambapo tayari ametembelea wilaya za Tanga Mjini, Pangani, Mkinga, Muheza, Lushoto, na Korogwe. Baada ya Handeni, anatarajiwa kuhitimisha ziara yake kesho katika Wilaya ya Kilindi.
MWISHO.
