Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
CCM YAIPA JIJI LA TANGA MWEZI MMOJA KUREKEBISHA SOKO LA MGANDINI

CCM YAIPA JIJI LA TANGA MWEZI MMOJA KUREKEBISHA SOKO LA MGANDINI


NA AMINA SAIDI, TANGA.

​Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Rajab Abdurhaman, ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha miundombinu ya soko la Mgandini inaboreshwa, ikiwemo kuondoa kero ya taka na matope ili kuimarisha hali ya usafi.

​Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa awali kuhusu kuboresha mazingira ya soko hilo.

 Katika ziara hiyo, Rajab amesisitiza umuhimu wa kuboresha maeneo ya kukusanyia taka kwa kujazwa kifusi, kurekebisha barabara za ndani, na kuhakikisha maji ya mvua yanaelekezwa kwenye mifereji ili kuepusha mafuriko yanayozua kero ya tope kwa wafanyabiashara na wananchi.

​Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Rajab amewapongeza viongozi wa Jiji, akiwemo Mstahiki Meya, kwa kuanza kuchukua hatua za awali za kusafisha soko hilo, Hata hivyo ametoa onyo kali kuwa hataki kusikia visingizio badala ya utekelezaji,huku akisisitiza kuwa ndani ya mwezi mmoja kuanzia Aprili 9 hadi Mei 9, anatarajia kuona mabadiliko makubwa ya vitendo.

​Mwenyekiti huyo pia ameeleza kutoridhishwa kwake na hali ya vyoo katika soko hilo, akibainisha kuwa huduma zilizopo hazitoshelezi mahitaji ya idadi kubwa ya watumiaji, jambo linalohatarisha afya za jamii.

 Amelitaka Jiji kutafuta suluhisho la kudumu la mfumo wa maji taka, huku akiwapongeza kwa kuanza mpango wa ujenzi wa choo kipya chenye matundu 12.

​Aidha, kiongozi huyo ameelekeza kuwepo kwa utaratibu maalum wa magari ya mizigo ili kupunguza msongamano ndani ya soko.

 Amependekeza magari yapaki nje ya soko na kuingia kwa zamu kushusha bidhaa, huku akiongeza kuwa Jiji la Tanga ni taswira ya mkoa na linapaswa kurejesha sifa yake ya zamani ya kuwa mji wa usafi na ustaarabu.

​Kwa upande wake, Naibu Meya wa Jiji la Tanga ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwanzange, Khalid Rashid, amesema kuwa Jiji lina mpango wa kuboresha njia za kupita ndani ya soko ili kuondoa changamoto ya matope wakati wa mvua.

 Amesema kuwa kazi hiyo ya uboreshaji wa miundombinu inatarajiwa kuanza rasmi ndani ya wiki moja.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3