JKCI YAANZA MCHAKATO WA UPANDIKIZAJI MOYO, YALENGA HUDUMA KUANZA IFIKAPO 2030
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI ) imetangaza kuanza rasmi mchakato wa kufanya upandikizaji wa moyo nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo
Akizungumza leo April 9, 2026 jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Peter Kisenge, amesema kuwa hatua ya awali imejikita katika kufanya upembuzi yakinifu ili kuhakikisha huduma hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.
“Kwa mwaka 2025 tumeanza mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu wa huduma ya upandikizaji wa moyo na tayari tumeunda kamati maalumu iliyoandaa dira ya namna huduma hii itakavyoanzishwa nchini,” amesema Dkt. Kisenge.
Amefafanua kuwa kamati hiyo imekamilisha rasimu ya mwongozo wa uanzishwaji wa huduma hiyo na kuikabidhi mwezi Januari mwaka huu, hatua inayofungua njia kwa maandalizi zaidi ya utekelezaji.
Aidha, amesema hatua inayofuata ni kuwapeleka wataalamu wa JKCI katika hospitali za kimataifa zinazotoa huduma za upandikizaji wa moyo ili kupata ujuzi na uzoefu wa vitendo.
“Tunatarajia ndani ya miaka mitano ijayo, yaani ifikapo mwaka 2030, JKCI iwe miongoni mwa hospitali zinazotoa huduma ya upandikizaji wa moyo duniani,” ameongeza.
Mpango huo unatarajiwa kupunguza gharama na usumbufu kwa wagonjwa waliokuwa wakisafiri nje ya nchi kutafuta huduma hiyo, huku ukiimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani na sekta ya afya kwa ujumla.



