Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TRA MOROGORO KUJA NA TAX CLUB SHULE ZA SEKONDARI

TRA MOROGORO KUJA NA TAX CLUB SHULE ZA SEKONDARI


 NA FARIDA MANGUBE MATUKIO DAIMA APP  MOROGORO 


Katika juhudi za kujenga kizazi chenye uelewa wa masuala ya kodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Morogoro ipo kwenye mpango wa kuanzisha vilabu vya kodi (Tax Club) katika shule za sekondari wilayani Kilosa, ikiwa ni hatua muhimu ya kukuza uzalendo na uwajibikaji wa kifedha miongoni mwa wanafunzi.


Meneja wa TRA wilaya ya Kilosa, Laston Makarlu, amesema Tax Club itasaidia kuwajengea wanafunzi uelewa sahihi kuhusu umuhimu wa kodi katika maendeleo ya taifa, ili waweze kuwa walipa kodi waadilifu pindi watakapoingia katika shughuli za kiuchumi. Alibainisha kuwa elimu hiyo itasaidia kuondoa dhana potofu zilizojengeka kwa baadhi ya wananchi kuhusu kodi.


Kwa upande wake, Bi. Emmaculatha Chagu Afisa Mwandamizi wa Elimu na Mawasiliano TRA Morogoro alieleza kuwa utoaji wa elimu ya kodi kuanzia ngazi ya chini ni mkakati sahihi utakaosaidia kujenga uelewa wa kudumu kwa wanafunzi. “Elimu ya mapato lazima ianzie chini ili kuwajenga vijana kuwa raia wanaotambua wajibu wao kwa taifa. Kuanzishwa kwa Tax Club kutawapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo na kujenga mtazamo chanya kuhusu ulipaji kodi,” alisema.


Aliongeza kuwa vitakapoanzisha vilabu hivyo vitasaidia pia kukuza uongozi, uwajibikaji na nidhamu miongoni mwa wanafunzi, huku vikitoa jukwaa la majadiliano na ubunifu kuhusu masuala ya uchumi na maendeleo ya nchi.


Pia Tax Club itasaidia kutoa elimu ya msingi kuhusu mfumo wa kodi, wajibu wa mlipa kodi, pamoja na mchango wa kodi katika kugharamia huduma za jamii kama elimu, afya na miundombinu.



Programu hiyo inatarajiwa kutekelezwa katika wilaya zote za Mkoa wa Morogoro, ambapo kwa sasa imeanza kwa kutoa elimu katika Wilaya za Gairo na Kilosa, huku maandalizi yakiendelea kuhakikisha Wilaya zote za mkoa huo yanafikiwa.


Zoezi hilo lilifanyika kwa ushirikiano wa maafisa kutoka TRA mkoa wa Morogoro, ambapo walitembelea shule mbalimbali zikiwemo Kimamba Sekondari na Mazinyungu Sekondari kuzungumza na walimu.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3