SUMAUJATA LINDI WATAKIWA KUWEKA KIPAUMBELE MALEZI BORA YA MTOTO
Mar 10, 2026
NA HADIJA OMARY
LINDI....Jumuiya ya Mashujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SUMAUJATA) Mkoa wa Lindi imetakiwa kuhakikisha masuala ya malezi ya mtoto yanazingatiwa na kupewa kipaumbele katika jamii, hususan kwa wazazi, walezi na wadau mbalimbali.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Mradi wa Mtoto Kwanza Mkoa wa Lindi, (Edger) Mapunda kutoka Kituo cha Msaada wa Wasaidizi wa Kisheria wa Wanawake Lindi,(LIWOPAC) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo mashujaa wa SUMAUJATA yaliyofanyika katika Halmashauri ya Mtama.
Katika mafunzo hayo, washiriki wamejengewa uwezo kuhusu masuala ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kuanzia umri wa miaka sifuri hadi nane, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kukua na kuendelea.
Mapunda amesema lengo la programu hiyo ni kuhakikisha mtoto anakuwa katika utimilifu wa ukuaji wake kupitia uwekezaji katika maeneo matano ya mfumo wa malezi jumuishi. Maeneo hayo ni pamoja na afya bora, lishe, malezi yenye muitikio, fursa za ujifunzaji wa awali pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto.
Amesema kuwa kuimarisha ushirikiano kati ya wadau mbalimbali, ikiwemo SUMAUJATA, katika utoaji wa huduma za malezi jumuishi kwa watoto kutasaidia kuongeza uwekezaji katika huduma za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) na kuwawezesha watoto kufikia Ukuaji wao timilifu
“Pamoja na mambo mengine, katika kikao hiki tumeweza kuweka maadhimio mbalimbali yatakayotuwezesha kutekeleza majukumu yetu. Miongoni mwa maadhimio hayo ni umuhimu wa kuwekeza katika malezi bora ya mtoto pamoja na matumizi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kuhamasisha jamii ipate uelewa juu ya programu hii,” amesema Mapunda.
Maadhimio mengine yaliyofikiwa ni pamoja na kushirikiana na wadau wengine katika kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, kuanzisha bonanza litakalotumika kutoa elimu kuhusu haki za watoto, wajibu wa wazazi na walezi, pamoja na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa malezi bora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SUMAUJATA Halmashauri ya Mtama, Mwalimu Irene Wemba amesema wamepokea mafunzo hayo kwa furaha kubwa kwani yanagusa moja kwa moja maisha ya jamii na yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na katika familia zao.
Amesema mafunzo hayo yana manufaa makubwa kwa halmashauri hiyo na yana matarajio ya kuleta matokeo chanya katika jamii wanazofanyia kazi.
Naye Mjumbe wa SUMAUJATA kutoka Shule ya Msingi Nang’aka, Mwalimu Fadhiri Kanduru amesema kupitia mafunzo hayo wameweza kujifunza mambo mengi ambayo hapo awali hawakuwa wakiyafahamu, na kwamba yamewapatia uzoefu utakaowasaidia katika kuwahudumia watoto na jamii kwa ujumla
Instagram@tanzaniaecdnetwork
Istagram @liwopac
@watotowetutunuyetu
MWISHOOO



