TAKUKURU YAREJESHA SERIKALINI SH. 119.1 MILIONI, NA MAGARI MANNE SINGIDA
Na Elisante John, Matukio Daima Media ,Singida.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mchini (TAKUKURU), imerejesha serikalini fedha zaidi ya Sh.119.1 milioni, na magari manne yakiwemo malori makubwa mawili ya shirika moja lisilokuwa na kiserikali mkoani Singida, yaliyouzwa kinyume cha utaratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Singida, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa, Petro Horombe, alisema mafanikio hayo ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/26, yametokana na juhudi za Taasisi hiyo kusimamia vema uwajibikaji, udhibiti wa vitendo vya rushwa, na ubadhirifu wa mali za umma.
Horombe alisema kuwa, magari manne yaliyorejeshwa ni mali ya shirika lisilo la kiserikali 'Sustainable Environmental Management Action' (SEMA), linalofanya kazi za kuimarisha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na usimamizi endelevu wa mazingira katika jamii, lenye makao yake makuu mkoani Singida,
Alifafanua kuwa magari hayo tayari yalikuwa yameuzwa na kuanza kutumika kwa mtu mmoja, likiwemo lori Isuzu Tipa Crane T 418 AED, Isuzu Tipa T 423 AED, Toyota Land Cruiser VX T 465 AED na Land Rover one ten 110 T412 AED, yote yakiwa tayari kwa mfanyabiashara huyo.
Alisema kurejeshwa kwa magari hayo ni hatua muhimu katika kuhakikisha mali za taasisi, kampuni na mashirika mbalimbali, bila kujali yanamilikiwa na serikali au binafsi yanayohudumia umma, zinatumika kwa uadilifu na kwa manufaa ya wananchi wote.
Kadhalika Horombe alisema kuwa, TAKUKURU imefanikiwa pia kurejesha kiasi cha Sh7.3 milioni, kutoka kwa mfanyabiashara mmoja, aliyetoa stakabadhi ya kughushi kwenye shughuli za biashara baina yake na serikali, hali iliyosababisha uchunguzi wa kina kufanyika, na fedha hizo zikarejeshwa serikalini.
“Rushwa bado ipo katika sekta ya umma na hata pia kwa sekta binafsi, hivyo ni wajibu wa kila taasisi na kila mwananchi kushiriki kikamilifu kuzuia na kudhibiti vitendo hivyo, kwa maslahi ya Taifa,” alisema Horombe na kuongeza kuwa,
"...katika kipindi hicho, pia TAKUKURU imefanya uchunguzi, chambuzi za mifumo na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji miradi ya maendeleo 25, yenye thamani ya Shilingi 5,177,915,609/=, katika sekta ya elimu, maji, Barbara, afya na utawala," alihitimisha Horombe.
Kutokana na kazi hiyo nzuri, baadhi ya wadau wa maendeleo na wananchi mbalimbali, wamepongeza juhudi za TAKUKURU katika kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, na kuhamasisha uwajibikaji katika jamii.
Baadhi ya wadau ni dereva bodaboda mwanamke Mary Muna, ambaye alisema elimu inayotolewa na TAKUKURU imesaidia wananchi kuelewa athari za rushwa na umuhimu wa kushirikiana na taasisi hiyo katika kufichua vitendo vya rushwa.
aidha Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida, Sadru Kamugisha, pamoja, mdau wa maendeleo Rashid Hamimu na mwalimu Hatima Msangi wa Shule ya Sekondari Senge, kwa pamoja walisema klabu za kupambana na rushwa mashuleni zimeanza kuzaa matunda kwa kuwajengea wanafunzi uelewa mpana zaidi kuhusu athari za rushwa na umuhimu wa uadilifu kwa jamii.



