MIKOKO : HADITHI YA UHALIBIFU , UHAI NA TUMAINI LA PWANI YA TANZANIA
Na Hadija Omary,Lindi
Asubuhi ya pwani huwa na utulivu wa kipekee. Mawimbi yanapogonga ufukwe kwa upole, sauti ya upepo hupenya katikati ya miti ya mikoko au tuseme, ilivyokuwa zamani. Leo, katika baadhi ya maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi, ukimya huo umechukua sura nyingine; ni ukimya unaoacha maswali mengi baada ya mikoko kupungua kwa kasi.
Kwa miaka mingi, jamii za pwani zimekuwa zikitegemea mikoko kama chanzo cha kuni, mbao za ujenzi, na hata kipato cha haraka kupitia biashara ndogo ndogo. Lakini utegemezi huo, uliokosa mipaka na usimamizi madhubuti, umegeuka kuwa tishio kubwa kwa uhai wa mikoko. Ukataji holela, ujenzi usiozingatia mazingira, na shughuli nyingine za kibinadamu vimeacha maeneo mengi yakiwa wazi, yakikosa kinga dhidi ya mmomonyoko wa ardhi na kupoteza mazalia ya samaki.
Ndipo hadithi mpya ya matumaini ilipoanza kuandikwa.
Katika viwanja vya Ilulu, Manispaa ya Lindi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na kampeni ya kitaifa ya upandaji miti, sauti za wadau wa mazingira zilijaa msisitizo wa mabadiliko.
Miongoni mwao ni Shirika la Earthlungs, ambalo limejipambanua kama kinara wa juhudi za kurejesha mikoko nchini.
Akizungumza katika tukio hilo, Mratibu wa Miradi wa shirika hilo, Husen Hassan, alieleza kwa msisitizo kuwa tangu waanze shughuli zao mwaka 2024, tayari wamepanda mikoko milioni 40, huku kiwango cha uhai wa miti hiyo kikiwa ni asilimia 85 hatua kubwa inayodhihirisha mafanikio ya juhudi hizo.
“Tulianza Mkoa wa Tanga, lakini sasa tupo pia Mkoa wa Pwani. Kwa sasa tunatekeleza miradi katika wilaya za Mkinga, Tanga Mjini na Pangani, pamoja na Bagamoyo. Malengo yetu ni kupanua zaidi hadi mikoa ya kusini ikiwemo Lindi na Mtwara,” alieleza Hassan.
Aliongeza kuwa mikoko ina uwezo mkubwa wa kupunguza hewa ukaa mara nne zaidi ya miti ya kawaida, jambo linaloifanya kuwa silaha muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
“Ni mti ulioathirika sana kutokana na ukataji mkubwa, ndio maana tukaanza nao kuokoa kile kinachopotea kwa kasi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Msimamizi Mkuu wa Operesheni za Misitu wa Earthlungs, John Logart, alifafanua mkakati wa kipekee wa shirika hilo kuweka jamii katikati ya suluhisho. Alisema asilimia 80 ya shughuli za mradi zinalenga kunufaisha jamii moja kwa moja.
“Tukiwa kwenye eneo la kazi, tunahakikisha wanajamii wanapata ajira. Hii inawafanya wawe walinzi wa mikoko wenyewe,” alisema. Aliongeza kuwa baada ya kurejesha maeneo ya mikoko, shirika linaanzisha shughuli mbadala za kiuchumi kama ufugaji wa nyuki, mbuzi na ulimaji wa uyoga ili kupunguza utegemezi wa moja kwa moja kwenye mikoko.
Simulizi hii inapata uhai zaidi kupitia ushuhuda wa Huruma David, Afisa wa Athari za Kijamii kutoka Earthlungs. Anaeleza jinsi maisha ya wanajamii yalivyobadilika.
“Hapo awali watu walikuwa wanakata mikoko ili kujipatia kipato. Lakini sasa tumewapa ajira wanapanda na kutunza mikoko, na mwisho wa mwezi wanapata mshahara,” alisema. “Leo hii, wana uwezo wa kulipia karo za shule, kununua chakula na mahitaji mengine bila kulazimika kuharibu mazingira.”
Katika ngazi ya uongozi wa mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, alieleza kuwa mkoa huo una zaidi ya hekta milioni 1.058 za misitu iliyohifadhiwa kisheria, ikijumuisha misitu ya taifa, vijiji, na ile ya mikoko kando ya Bahari ya Hindi.
Alibainisha kuwa mikoko iliyohifadhiwa katika mkoa huo pekee ina ukubwa wa zaidi ya hekta 27,660 katika wilaya za Lindi na Kilwa, huku juhudi zikiendelea za kupanda angalau hekta 10 kila mwaka ili kuimarisha uhifadhi huo.
Katika hatua ya kuonyesha dhamira ya serikali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, aliongoza zoezi la upandaji wa miche 120 ya mikoko katika fukwe za Machole, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho hayo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Waziri Kijaji alisema Tanzania ina takribani hekta 158,100 za misitu ya mikoko, akisisitiza umuhimu wake katika uchumi wa taifa na uhai wa sayari.
“Mikoko ni muhimu sana. Ina uwezo mkubwa wa kufyonza gesi ya hewa ukaa, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi. Lakini pia ni mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini,” alisema. “Tukiiharibu mikoko, tunaharibu pia vyanzo vya chakula na kipato kwa jamii zetu.”
Aliongeza kuwa mikoko pia husaidia kuzuia mmomonyoko wa ardhi katika maeneo ya pwani, hivyo kuilinda miundombinu na makazi ya watu.
Kadri jua lilivyozama katika anga la Lindi siku hiyo, haikuwa tu mwisho wa maadhimisho bali mwanzo wa ahadi mpya, ahadi ya kurejesha kile kilichopotea. Kutoka kwenye mikono ya wanajamii waliokuwa wakikata mikoko jana, hadi kuwa walinzi wake leo, simulizi ya mikoko inaendelea kuandikwa upya.
Na katika kila mche unaopandwa, kuna tumaini la mazingira salama, uchumi endelevu, na kizazi kijacho kinachorithi bahari yenye uhai mpya.






