Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SHEKHE SINGIDA APIGA WALIMU WA MADRASA 'VIJIWENI'

SHEKHE SINGIDA APIGA WALIMU WA MADRASA 'VIJIWENI'

 

‎ 

Na Elisante John, Singida

‎Shekhe wa Mkoa wa Singida, Alhaji Issah Nassoro, amepiga marufuku walimu wa elimu ya dini ya Kiislamu (madrasa) wanaotumia muda mwingi vijiweni na kwenye kahawa wakijadili na kuwakosoa viongozi wa Taasisi za dini, akitaka kujikita zaidi kufundisha na kulea maadili ya wanafunzi, ambao ndio viongozi na waimini wa kesho.


‎Akizungumza leo Machi 22, 2026 katika Baraza la Eid el-Fitr la Mkoa lililofanyika kmUwanja wa Bombadia mjini Singida, Shekhe Nassoro alisema tabia hiyo inachochea migogoro na kudhoofisha umoja ndani ya jamii ya Kiislamu.

‎Alisema badala ya walimu hao kutumia muda wao katika majadiliano yasiyo na tija, wanapaswa kuelekeza nguvu katika kuwanoa wanafunzi kwa misingi ya dini na maadili mema kwa manufaa ya jamii na taifa hapo baadaye.


‎Kwa mujibu wa Shekhe huyo, baadhi ya walimu wamekuwa wakijihusisha na majungu na kutoa kauli zinazodhalilisha uongozi wa taasisi za ibada, wakidai kuwa hauwafai au hauwakilishi ipasavyo wakazi wa Singida.

‎“Walimu wote wajikite katika kufundisha dini yetu. Anayetaka kushika nafasi ya uongozi ajipange kwa utaratibu unaostahili, si kwa kuchochea maneno ya mitaani,” alisema Shekhe Nassoro.

‎Katika hatua nyingine, aliwataka viongozi wa taasisi za Kiislamu zilizosajiliwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mipaka ya usajili wao, ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.


‎Aidha, aliwahimiza waumini wa Kiislamu mkoani humo kuimarisha umoja na mshikamano, akieleza kuwa mafanikio ya taasisi zao yanategemea ushirikiano na kuheshimiana miongoni mwao.

‎Kwa upande wake, Kadhi wa Mkoa wa Singida, Mbaraka Ally Esya, alisema tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, amejikita katika kutatua migogoro ya ndoa kwa njia ya usuluhishi badala ya kutoa adhabu za moja kwa moja.


‎Aliongeza kuwa pale ambako suluhu hushindikana, basi hatua za kisheria huchukuliwa, ikiwemo kutoa talaka kwa kufuata taratibu, huku wahusika wakitakiwa kugharamia uendeshaji unaofikia Sh150,000.


‎Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, mgeni rasmi Shabani Mong’ong’o aliwataka viongozi na waumini kuimarisha umoja, kudumisha amani na upendo katika nyumba za ibada, sambamba na kuwekeza katika elimu ya dini na masomo ya kawaida kwa watoto wai, ili kuwaandaa vema kwa maisha yao ya baadaye.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3