AJALI YA BASI LA SHABIBY NA LORI IRINGA YAUA 6
May 8, 2026
TAZAMA VIDEO BOFYA LINK HII
Watu sita wamefariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Shabiby aina ya Youtong likiendeshwa na Michael Mbugi likitokea Dodoma kwenda Mbeya na kupata ajali katika kijiji cha Tanangozi, Kata ya Mseke mkoani Iringa, alfajiri ya leo Mei 8, 2026 baada ya kugongana na lori la vinywaji aina ya FAW.
Akithibitisha kutoa kwa ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa SACP Allan Bukumbi alisema ajali hiyo imetokea majira ya saa 8 usiku huku chazo kikielezwa kuwa ni dereva wa lori kushindwa kulimudu gari lake kwenye mteremko mkali na kuhamia upande wa pili na kugongana uso kwa uso na basi kampuni ya Shabiby.
Kamanda Bukumbi alisema kuwa dereva wa lori hilo lenye namba za usajili T 143, EAF mali ya Said Salim Mohamed ya Tanga alifariki hapo hapo ambaye alikuwa akitokea mbeya kuelekea Dodoma.
“lori hilo liligongana na basi la shabiby lililokuwa likiendeshwa na Michael Mbugi ambaye alikuwa akitokea Dodoma Kuelekea Mbeya naye alifariki hapo hapo, ambapo katika ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu watatno na majeruhi 28”
“majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kwa matibabu ambapo wanaendelea kupewa matibabu, na miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ambapo ndugu zao watafika kutmbua maiti kwa ajili ya hatua za mazishi”alisema
Akizungumza na wanahabari, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela amesema hospitali hiyo imepokea majeruhi 28 waliotokana na ajali hiyo pamoja na miili ya watu watano waliofariki dunia.
Dk Mwakalebela amesema kati ya majeruhi hao, wanaume ni 16 wakiwemo watoto wanne, huku wanawake wakiwa 12.
Kwa mujibu wa daktari huyo, mmoja wa majeruhi mwenye asili ya Asia amelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) kutokana na kuumia zaidi kichwani.
"Majeruhi wengine hali zao ni mbaya na wanaendelea kupatiwa matibabuWapo waliopata majeraha ya kichwa, mmoja jicho limetoka na kuna taratibu zinaendelea huyo mmoja ambaye ameumia sana kumhamishia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi," amesema Dk Mwakalebela.
Dk Mwakalebela ameongeza kuwa watu 11 waliopata majeraha madogo tayari wameruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu.
Hata hivyo idadi ya vifo imeongezeka baada ya majeruhi mwingine Kijana mwenye asili ya Asia kufariki dunia hivyo idadi kufikia watu 6
Wakizungumza baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wanasema kuwa walipata taarifa za ajali majira ya saa 7 usiku na baade kufika katika hospitali ya rufaa kujua hali za wagonjwa na ndugu waliokuwa katika ajali hiyo.
“Mimi nilikuwa nimewasindikiza ndugu zangu kupanda basi usiku wa saa 7 walikuwa wanaelekea Mbeya baada ya kupanda haikupita muda mrefu wakanipigia kuwa wamepata ajali hivyo wanapelekwa katika hospitali ya Iringa na mimi nikafika hospitali kuwajulia hali na mpaka sasa wamepatiwa matibabu na wanaendelea vizuri”alisema shuhuda
Kwa upande wake Rusiano Mbosa ambaye pia ni shuhuda alisema kuwa alifika katika hospitali ya rufaa saa 8:40 baada ya kupata taarifa kuwa basi limepata ajali hivyo wakafika hospitali kwa ajili ya kuwaona ndugu zao.

.jpg)

