SHULE ZOTE ZIWE NA BUSTANI ZA MBOGA MBOGA – DC ITUNDA
Na Matukio DaimaApp,
Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, amewaagiza maafisa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuhakikisha wanasimamia zoezi lakuanzisha na kuimarisha bustani za mboga mboga shuleni ili kuboresha lishe ya wanafunzi.
Mhe. Itunda ametoa agizo hilo February 26,2026 wakati akizungumza katika kikao cha tathmini ya lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, baada ya kupokea ripoti ya hali ya lishe kutoka katika kata zote 28 za wilaya hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa mboga mboga ni muhimu katika ukuaji na maendeleo ya mtoto, hivyo ni lazima ziwe sehemu ya chakula kinachotolewa shuleni.
“Lishe bora ni msingi wa afya na maendeleo ya mtoto. Ni muhimu kuhakikisha kila shule inakuwa na bustani ya mboga mboga ili wanafunzi wapate chakula chenye virutubisho vya kutosha,” amesema Mhe. Itunda.


