Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DKT. TULIA AIKUMBUSHA HALMASHAURI YA JIJI LA MBEYA KUTENGA BAJETI KUONGEZA MIRADI

DKT. TULIA AIKUMBUSHA HALMASHAURI YA JIJI LA MBEYA KUTENGA BAJETI KUONGEZA MIRADI

Na Matukio Daima Media Media 

Mbeya

Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, ameikumbusha Halmashauri ya Jiji la Mbeya pamoja na viongozi wa serikali kuhakikisha wanatenga bajeti maalum kwa ajili ya kuongeza miradi ya ujenzi wa madarasa ya kidato cha tano na sita.

Dkt. Tulia amesema kuwa ipo haja ya kubaini shule za sekondari zitakazonufaika na miradi hiyo, ili ziweze kujipatia mapato kupitia ada zitakazolipwa na wanafunzi watakaojiunga katika madarasa mapya.


Ametoa kauli hiyo Februari 26, 2026 wakati akishiriki kikao cha Baraza la Bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Mhe. Dor Mohamed Issa. Kikao hicho kilifanyika katika ofisi za Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Dkt. Tulia amesema kuwa mapato yatakayopatikana kupitia miradi hiyo yanaweza kusaidia kukarabati baadhi ya shule za msingi zenye miundombinu duni, ikiwemo kutatua changamoto ya upungufu wa madawati, kwa kushirikiana na wadau wa elimu.

Aidha, ameipongeza ofisi ya Mstahiki Meya kwa kufanya ukusanyaji mzuri wa mapato, hatua inayowezesha serikali kutekeleza malengo na matarajio ya wananchi.


Katika kikao hicho, Dkt. Tulia pia aliomba uongozi wa halmashauri kuhakikisha kuwa miundombinu katika eneo jipya la wafanyabiashara wa Soko la Uyole ya Kati, lililopo Kata ya Iganjo, inaandaliwa mapema kabla ya wafanyabiashara kuhamishwa kupisha ujenzi wa barabara. Amesema haipendezi wafanyabiashara kuhamishwa na kufika eneo jipya kisha kusubiri miundombinu kukamilishwa.


Kuhusu miundombinu ya barabara, Dkt. Tulia ametaka watumishi wa TARURA kusimamia kwa umakini miradi ya ujenzi wa barabara, akibainisha kuwa changamoto ya barabara kuharibika muda mfupi baada ya kujengwa inawasumbua wananchi. Ametaka wakandarasi kuhakikisha barabara zinajengwa kwa viwango vinavyotakiwa.


Mwisho wa hotuba yake, Dkt. Tulia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuruhusu matumizi ya fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na ukarabati wa miundombinu. Amesema hatua hiyo imeongeza mapato na kuchangia mafanikio ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya.


Mwisho.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3