MGOMBEA UDIWANI CCM KATA YA SHIWINGA ASHINDA
Na Moses Ng'wat, Mbozi.
MGOMBEA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Menati Mzumbwe, ameibuka mshindi katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Shiwinga, Wilaya ya Mbozi, baada ya kupata kura 5,030 kati ya kura halali 5,210 zilizopigwa.
Matokeo hayo yametangazwa FEBRUARI 26, 2026 na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Shiwinga, Selestin Luambano, mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu kura.
Kwa mujibu wa Luambano, jumla ya wapiga kura waliojiandikisha katika kata hiyo ni 6,852. Kura zilizopigwa ni 5,229, ambapo kura halali zilikuwa 5,210 na kura 19 ziliharibika.
Katika matokeo hayo, wagombea wengine walipata kura kama ifuatavyo,Matias Dulle (ADC) kura 62, Elly Shitindi (ADA-TADEA) kura 8, Neema Daud (UPDP) kura 15, Neema Abadallah (UMD) kura 22, Emily Siwale (SAU) kura 24, Mussa Dulle (Chama-Makin) kura 32 na Cosam Mwakyusa (TLP) kura 17.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo, mgombea wa UPDP, Neema Daud, amesema anakubaliana na matokeo yaliyotolewa na kuipongeza tume kwa usimamizi mzuri wa uchaguzi huo.
Amesema tume ilikuwa wasikivu na ilitoa ushirikiano kwa wagombea wote pale changamoto zilipojitokeza bila upendeleo wowote.
Ameongeza kuwa kura alizopata kila mgombea, hata kama ni chache, ni haki yake kwa mujibu wa utaratibu wa kidemokrasia.
Kwa upande wake, diwani mteule, Mzumbwe amewashukuru wananchi kwa kumuani na kumpatia kura za kishindo na k7ahidi kushirikiana katika kuleta maendelea katika kata hiyo.
Uchaguzi huo umeitishwa kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Lusekelo Mwalukomo, kilichotokea Novemba 26, 2025, baada ya kunywa maji ya betri, zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo.
Mwisho.
