MADHARA YA WANAWAKE NA WASICHANA KUTUMIA P2
Na Catherin Kilwale (UoI), Matukio Daima Media
Daktari wa Zahanati ya Ngome, iliyopo Kata ya Kihesa mkoani Iringa, John Mlunguza, ameonya juu ya matumizi holela ya dawa za dharura za kuzuia mimba maarufu kama P2, akieleza kuwa matumizi yasiyo sahihi yanaweza kusababisha madhara kiafya kwa wanawake na wasichana.
Akizungumza na gazeti hili, Dk. Mlunguza alisema P2 ni njia ya dharura ya uzazi wa mpango na si mbadala wa njia za kawaida za uzazi wa mpango. Alibainisha kuwa baadhi ya wasichana na wanawake hutumia dawa hiyo mara kwa mara wakiamini ni njia rahisi ya kuzuia ujauzito, bila kufahamu athari zinazoweza kujitokeza.
“Matumizi ya mara kwa mara ya P2 yanaweza kusababisha mvurugiko wa homoni, maumivu ya kichwa, maumivu ya matiti pamoja na hedhi zisizo na mpangilio kwa muda mrefu aidha, matumizi yasiyo sahihi yanaweza kupunguza ufanisi wa dawa hiyo katika kuzuia mimba,” alisema Dk. Mlunguza.
Kwa upande wake, mkazi wa Kihesa, Getruda Bulinje, alisema wanawake na wasichana wengi hutumia P2 kwa kuzingatia mahitaji ya muda mfupi bila kufikiria madhara ya baadaye.
“Baadhi ya wanawake na wasichana huona ni njia rahisi ya kuepuka ujauzito bila kuzingatia athari zinazoweza kujitokeza baadaye ni muhimu kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kutumia dawa yoyote ya uzazi wa mpango,” alisema Bulinje.
Naye Vignes Pius, pia mkazi wa Kihesa, alitoa wito kwa wanawake na wasichana kufika katika vituo vya afya kupata elimu sahihi kuhusu uzazi wa mpango badala ya kutumia dawa bila ushauri wa wataalamu wa afya.
“Ni vyema kufika kituo cha afya ili kupata ushauri na kuchagua njia sahihi na salama ya uzazi wa mpango matumizi yasiyo sahihi ya dawa yanaweza kuleta madhara kama maumivu makali ya kichwa na kizunguzungu,” alisema Pius.
Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa elimu sahihi kuhusu uzazi wa mpango ni muhimu katika kulinda afya ya mwanamke na kuzuia madhara yanayoweza kuepukika.
