Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 SABABU ZA UWEPO WA WATOTO WA MTAANI

SABABU ZA UWEPO WA WATOTO WA MTAANI

Na Easter Kameta (UoI),Matukio Daima Media 

 Baadhi ya wananchi mkoani Iringa wameeleza vyanzo mbalimbali vinavyochangia ongezeko la watoto wa mtaani pamoja na changamoto wanazokumbana nazo watoto hao katika maisha yao ya kila siku.

Akizungumza na Matukio Daima Media Samwel Joshua amesema manyanyaso kutoka kwa wazazi au walezi ni miongoni mwa sababu zinazopelekea watoto kukimbia makazi yao na kuishi mitaani.

“Manyanyaso kutoka kwa wazazi au walezi yanaweza kumfanya mtoto kuondoka nyumbani. Pia umaskini na ukosefu wa mahitaji ya msingi huwafanya watoto kutafuta maisha mbadala mitaani,” alisema Joshua.

Kwa upande wake, John Juma alieleza kuwa mimba za utotoni na migogoro ya kifamilia ni chanzo kingine cha tatizo hilo. 

Alisema kuwa migogoro ya mara kwa mara kati ya wazazi, ikiwemo kutengana au talaka, huathiri ustawi wa mtoto na wakati mwingine humlazimu kuondoka nyumbani.

“Mimba za utotoni na migogoro ya kifamilia huchangia watoto kuishia mtaani. Wazazi wanapotengana au kugombana mara kwa mara, mtoto hukosa malezi bora na kuamua kukimbilia mtaani,” alisema Juma.

 Every Yuda alitaja vifo vya wazazi au walezi vinavyotokana na maradhi au ajali kuwa sababu nyingine inayochochea ongezeko la watoto wa mtaani.

“Wazazi wanapofariki kwa magonjwa kama UKIMWI au ajali na kuwaacha watoto bila msaada wa kifamilia, watoto hao hukosa mahitaji na malezi stahiki na kujikuta wakihangaika mitaani,” alieleza Yuda.

Mbali na sababu hizo, Letsia Lubusi alizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo watoto wa mtaani, ikiwemo ukosefu wa elimu, magonjwa kama utapiamlo, unyanyasaji wa kijinsia na kimwili, pamoja na athari za matumizi ya dawa za kulevya.

“Watoto wa mtaani hukosa fursa ya elimu, hukumbwa na magonjwa, na wakati mwingine hujiingiza katika makundi ya kihalifu kama wizi na vitendo vya ukatili kutokana na mazingira wanayoishi,” alisema Lubusi.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3