Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAHITIMU TIA MWANZA WAHIMIZWA UWAJIBIKAJI, UADILIFU

WAHITIMU TIA MWANZA WAHIMIZWA UWAJIBIKAJI, UADILIFU

 



Na CHAUSIKU SAID -MATUKIO DAIMA MWANZA.


Wahitimu 1,402 wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mwanza, wametakiwa kutumia maarifa na ujuzi walioupata chuoni hapo kukabiliana na changamoto za maisha kwa kujijenga kikamilifu katika maendeleo ya taifa kwa kuzingatia misingi ya uadilifu na uwajibikaji.


Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, wakati akizungumza katika mahafali ya 24 ya TIA, Kampasi ya Mwanza, yaliyofanyika Novemba 27, 2026, ambapo ameeleza kuwa wahitimu hao wanatoka katika ulimwengu wa kujifunza na kuingia katika ulimwengu wa kazi, biashara, uongozi na uwajibikaji.


Amesema katika safari yao mpya wanapaswa kuzingatia madaraja matatu muhimu yatakayowawezesha kufikia mafanikio, ambayo ni miundombinu inayowaunganisha wananchi na kufungua fursa za kiuchumi, maarifa wanayoyapata kupitia elimu na ujuzi pamoja na uadilifu na uwajibikaji.




Naibu Waziri Luswetula amesema daraja la uadilifu na uwajibikaji ni muhimu zaidi kwa kuwa linaunganisha mtaalamu na jamii inayomzunguka, mfanyabiashara na mteja wake pamoja na wananchi na taifa kwa ujumla.


Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu na uchumi, ikiwemo Mkoani Mwanza, ambapo kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa mageuzi ya Kiuchumi imewekeza takribani Sh Bil 7.25 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 336.


Akizungumzia maendeleo ya TIA Kampasi ya Mwanza, Luswetula ameipongeza taasisi hiyo kwa kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, hatua iliyochangia ongezeko la udahili wa wanafunzi kutoka 1,719 mwaka wa masomo 2024/2025 hadi kufikia 4,584 mwaka 2026/2027.


Pia ameipongeza TIA kwa kutekeleza mpango wa kukuza uwezo wa wanafunzi kitaaluma ambao umefikia takribani wanafunzi 2,500 tangu mwaka 2022, pamoja na kuanzisha mashindano ya mawazo bunifu ya kibiashara yanayolenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kubuni fursa za kiuchumi.



"Naipongeza TIA kwa mpango wa ukuzaji wa wanafunzi kitaaluma uliowafikia takribani wanafunzi 2,500 tangu mwaka 2022, pamoja na mashindano ya mawazo bunifu ya kibiashara ambapo mshindi wa kwanza atapata fursa ya kwenda nchini China au Urusi kujifunza zaidi," amesema Luswetula.


Amesema jitihada hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inayosisitiza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuchochea maendeleo ya taifa.


Amewahimiza viongozi wa TIA kuendelea kuunga mkono mawazo bunifu ya wanafunzi ili yaweze kukua na kuwa biashara zitakazozalisha ajira kwa wahitimu wengine na wananchi kwa ujumla.


"Wahitimu, Serikali imewezesha miundombinu na TIA imewapatia maarifa. Endeleeni kujifunza kwa sababu cheti ni mwanzo wa safari na si mwisho wake," amesisitiza.




Kwa upande wake, Afisa mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania, Profesa William Pallangyo, amesema jumla ya wahitimu 1,402 wamehitimu katika kampasi hiyo, ambapo wanawake ni 713 sawa na asilimia 50.7 na wanaume ni 689 sawa na asilimia 49.3.


Amesema wahitimu hao wametoka katika fani mbalimbali zikiwemo Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Rasilimali Watu, Masoko na Uhusiano wa Umma pamoja na Usimamizi wa Biashara.


Ameeleza kuwa wahitimu wa Kampasi ya Mwanza ni asilimia 9.6 ya wahitimu wote wa TIA kwa mwaka huu ambao ni 14,613 kutoka kampasi mbalimbali nchini.


Amesema mahafali hayo yanaweka historia kwa Kampasi ya Mwanza kutokana na kuhitimisha kundi la kwanza la wahitimu wa Shahada ya Ualimu katika Uhasibu na Biashara.



Akizungumzia mafanikio ya kampasi hiyo, Pallangyo amesema idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa asilimia 47.7 kutoka 3,103 mwaka wa masomo 2025/2026 hadi kufikia 4,584 mwaka 2026/2027, ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,481.



Amesema ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa wanafunzi wanaonufaika na mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).


Amefafanua kuwa wanafunzi wanufaika wa mikopo wameongezeka kutoka 1,364 mwaka 2025/2026 hadi kufikia 2,503 mwaka 2026/2027, sawa na ongezeko la wanafunzi 1,139 au asilimia 83.5.


Aidha, amesema thamani ya mikopo hiyo imeongezeka kutoka Sh milioni 98.43 mwaka 2025/2026 hadi kufikia Sh bilioni 2.008 mwaka 2026/2027, hatua inayoonesha jitihada za Serikali kuhakikisha wanafunzi wengi wenye sifa wanapata fursa ya elimu ya juu bila vikwazo vya kifedha.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TIA, Profesa Jehovaness Aikaeli, ameishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwa mstari wa mbele katika kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia katika taasisi hiyo.


Amesema bodi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutoa ushauri wa kimkakati kwa Waziri wa Fedha ili maendeleo ya TIA yaendane na sera, vipaumbele na mahitaji ya taifa, huku ikisisitiza ubora wa elimu, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3