JF MEDICARE SPECIALIZED POLYCLINIC YASOGEZA HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA IRINGA.
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
IRINGA. Wananchi wa Mkoani Iringa sasa wana fursa ya kupata huduma za matibabu ya kibingwa, vipimo vya maabara na ultrasound kupitia kituo cha JF Specialized Polyclinic kilichopo mjini Iringa, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika hospitali kubwa nje ya mkoa.
Akizungumza na Matukio Daima Media, mwakilishi wa kituo hicho, Lacia Salum, alisema kliniki hiyo imeanzishwa kwa kuzingatia uhitaji mkubwa wa huduma za madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto, ambao awali wananchi wengi walilazimika kuwatafuta katika maeneo mengine.
Alisema pamoja na huduma za magonjwa ya wanawake na watoto, kituo hicho pia kina madaktari bingwa wa mifupa, macho na magonjwa ya ndani, ili kuwapatia wananchi huduma mbalimbali za kibingwa karibu na makazi yao.
Kwa upande wake, Daktari Mkuu wa JF Medicare Specialized Polyclinic, Eric Masawe, alisema kituo hicho kinatoa huduma za madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani (Internal Medicine), wanawake (Gynecology), watoto (Pediatrics), pamoja na vipimo vya maabara na ultrasound za aina mbalimbali.TAZAMA MAHOJIANO BOFYA LINK HII
Alifafanua kuwa kituo hicho kinapokea wagonjwa wanaotumia bima za afya pamoja na wale wanaolipia huduma kwa fedha taslimu, hivyo kuwapa wananchi wenye mahitaji tofauti nafasi ya kupata matibabu.
Alisema huduma za kliniki zinapatikana kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa nne usiku, huku huduma za madaktari bingwa zikipatikana kwa ratiba maalumu, ikiwemo siku za mwisho wa wiki.
Aidha, uongozi wa kituo hicho umewahakikishia wananchi wa Manispaa ya Iringa na maeneo jirani kuwa watapata huduma zenye viwango bora, zikiwemo uchunguzi, vipimo, matibabu na dawa.
Kuanzishwa kwa huduma hizo kunatajwa kuwa fursa muhimu kwa wananchi, hususan wagonjwa wanaohitaji matibabu ya mifupa kufuatia ajali au changamoto nyingine za kiafya, ambao wakati mwingine hulazimika kusafiri kwenda hospitali kubwa kama Hospitali ya Benjamin Mkapa au vituo vingine vya kibingwa.
JF Medicare Specialized Polyclinic inapatikana Iringa mjini, mkabala na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, jengo la Asali, ghorofa ya pili.
MWISHO

