Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TIMU 28 ZASHIRIKI LIGI YA TAIFA YA KIKAPU DODOMA,betPawa YADHAMINI MPIRA WA KIKAPU,

TIMU 28 ZASHIRIKI LIGI YA TAIFA YA KIKAPU DODOMA,betPawa YADHAMINI MPIRA WA KIKAPU,

 

Na Lilian Kasenene,Morogoro

Matukio Daima Media 

TIMU 28 za mpira wa kikapu kutoka mikoa mbalimbali nchini zinashiriki mashindano ya Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL), yaliyoanza rasmi jijini Dodoma.


Katika mashindano hayo, timu 16 zinashiriki upande wa wanaume na timu 12 upande wa wanawake, huku kila timu ikijipanga kutetea ubingwa au kufanya vizuri katika michuano ya mwaka huu.

Mashindano hayo yameanza Novemba 28 na yanatarajiwa kuhitimishwa Desemba 8 mwaka huu katika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma. 


Hamasa ya zawadi za fedha taslimu kwa washindi wa kila mechi, zinazotolewa na betPawa kupitia programu ya Locker Room Bonus, inaongeza msisimko na ushindani katika michuano hiyo.


Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Kamishna wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Robert Manyerere, alisema michuano hiyo ni mwendelezo wa hatua za mashindano yanayoanzia ngazi ya vilabu katika mikoa, kisha kanda, kabla ya timu zilizofuzu kushiriki mashindano ya taifa.


Alisema mshindi wa michuano hiyo atapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya ngazi ya juu zaidi, huku timu zitakazoshika nafasi ya pili na ya tatu zikiwakilisha nchi katika mashindano ya Zone Five ya Afrika Mashariki.


Aidha, Manyerere alisema mashindano hayo yanadhaminiwa na betPawa kupitia programu yake ya Locker Room Bonus, ambayo inatoa fedha moja kwa moja kwa timu zinazoshinda mechi.


Kwa upande wake, Rais wa mabingwa mara mbili mfululizo wa ligi hiyo kwa wanawake, Fox Divas ya mkoani Mara, ambaye pia ni Mbunge, Esther Matiko, ameiomba Serikali kuongeza uwekezaji katika mchezo wa mpira wa kikapu na kuwataka wadhamini zaidi kujitokeza kuunga mkono mchezo huo.

Matiko alisema mpira wa kikapu nchini unaendelea kukua na kwamba taasisi binafsi zikiwekeza katika mchezo huo hazitajutia uamuzi huo. Hata hivyo, alibainisha kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa viwanja, hususan katika ngazi za chini, ikiwemo shule za msingi.


"Cha muhimu hapa ni kuanzia kwenye halmashauri kujenga viwanja rafiki, hata kwa kuanzia kujenga viwanja vya zege," alisema Matiko.


Naye Nahodha wa timu ya Stain Worries ya jijini Dar es Salaam, Brian Mramba, alisema timu yao imejipanga vizuri kwa msimu huu, huku akitoa wito kwa wadau na wadhamini mbalimbali kujitokeza kuunga mkono mchezo wa mpira wa kikapu.


Kwa upande wake, Mwakilishi wa betPawa, Rose Kishimba, alisema kampuni hiyo imeamua kudhamini moja kwa moja mchezo huo kwa lengo la kuwasaidia wachezaji kujikimu, hususan vijana ambao wamekuwa wakitumia muda na rasilimali zao kushiriki mashindano hayo.

Alisema fedha zinazotolewa kupitia programu hiyo zinawasaidia wachezaji kugharamia mahitaji mbalimbali, ikiwemo nauli na ununuzi wa vifaa vya michezo.

"Tangu tulipoanza kufadhili mchezo huu, kumekuwa na mabadiliko makubwa kwa wachezaji, ikiwemo kuongezeka kwa morali na hamasa ya timu nyingi kutaka kushinda na kucheza kwa kiwango cha juu," alisema Kishimba.

......



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3