MVUA MILIMA YA ULUGURU ZAONGEZA MAJI MTO RUVU,WAMI YAKABILIWA NA UPUNGUFU
Na Matukio Daima Media, Morogoro
Mvua zinazonyesha katika Safu za Milima ya Uluguru zimeendelea kuwa kichocheo cha ongezeko la maji katika Mto Ruvu, tofauti na Mto Wami ambao kiwango chake kimeendelea kushuka kutokana na upungufu wa mvua katika maeneo ya milima inayochangia maji yake.
Taarifa ya Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu inaonesha kuwa kiwango cha maji katika uwanda wa chini wa Mto Ruvu kimefikia lita 16,775 kwa sekunde, huku chanzo chake katika Safu za Milima ya Uluguru kikiwa na lita 13,699 kwa sekunde.
Ongezeko hilo limewezesha mahitaji ya maji kwa matumizi mbalimbali kuendelea kutimizwa, yakiwemo ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), RUWASA na kanda za viwanda.
Hali ni tofauti kwa Mto Wami, ambapo kiwango cha maji kwa sasa ni lita 7,917 kwa sekunde na kinaendelea kupungua kutokana na uhaba wa mvua katika Milima ya Chenene, Nguu, Ukaguru na Rubeho.
Pamoja na kupungua kwa kiwango hicho, maji yaliyopo bado yanatosheleza mahitaji ya DAWASA, Shamba la Bagamoyo Sugar na Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Katika kipindi cha siku 10 zijazo, utabiri unaonesha mito yote miwili inatarajiwa kushuhudia upungufu zaidi wa maji kutokana na mwenendo wa mvua katika maeneo yake ya vyanzo.
Hata hivyo, hakuna viashiria vya mafuriko vilivyobainika katika maeneo mbalimbali ya Mito Ruvu na Wami.
Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa maji na kutoa taarifa kwa wadau na wananchi kuhusu mabadiliko yoyote yatakayojitokeza.
Mwisho
