QWARAY ONDOENI RUSHWA, URASIMU KUREJESHA IMANI YA WANANCHI
Nov 26, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media DODOMA
WATUMISHI wa umma wametakiwa kuondoa vitendo vya rushwa, urasimu na matumizi mabaya ya madaraka katika maeneo yao ya kazi ili kuboresha utoaji wa huduma na kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, wakati akifungua Kikao Kazi cha Saba cha Kubadilishana Uzoefu kati ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma katika utumishi wa umma.
Qwaray amesema utoaji wa huduma kwa wananchi ni wajibu wa watumishi wa umma na haupaswi kuhusishwa na upatikanaji wa rushwa, akisisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, weledi na kuzingatia sheria.
Amesema vitendo vya rushwa na urasimu vinapopewa nafasi katika ofisi za umma, wananchi hukosa huduma wanazostahili na kupoteza imani kwa Serikali, jambo linaloweza kudhoofisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo ya taifa.
“Wananchi wanapaswa kutambua kuwa kupata huduma si lazima watoe rushwa, na sisi watumishi tunapaswa kutambua kuwa kutoa huduma ni wajibu wetu, si mpaka upewe rushwa,” amesema.
Na Kuongeza "tabasamu linalotarajiwa kuonekana katika nyuso za Watanzania, kama alivyosisitiza Rais Samia Suluhu Hassan, litapatikana pale wananchi watakapohudumiwa kwa wakati, kuondolewa urasimu na kuheshimiwa wanapofika katika ofisi za umma, " Amesema Qwaray.
Amesema watumishi wa umma wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila vikwazo vinavyosababishwa na mienendo isiyozingatia maadili, akiwataka kuwa sehemu ya suluhisho badala ya kuwa chanzo cha malalamiko ya wananchi.
Qwaray amesema pamoja na Serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali katika usimamizi na utoaji wa huduma, bado taarifa za ukiukaji wa maadili zinaendelea kujitokeza katika taasisi mbalimbali.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni rushwa, uvujishaji wa siri za Serikali, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma, hujuma dhidi ya miradi ya maendeleo, matumizi ya lugha zisizo na staha, upendeleo na ukosefu wa uzalendo.
Amesema hali hiyo inahitaji taasisi simamizi za maadili kuongeza ushirikiano, kujenga uwezo kwa watumishi na kuimarisha mifumo ya kuzuia na kushughulikia vitendo vinavyokiuka maadili ya utendaji na taaluma.
Katika hatua nyingine, amesema Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora imepanga kuanzisha katika mwaka huu wa fedha programu za maadili zitakazojumuishwa katika taasisi za umma ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia watumishi katika maeneo yao ya kazi kupitia njia rasmi.
Amewataka viongozi na taasisi simamizi za maadili kuweka kipaumbele katika programu hizo na kuhakikisha wanakuwa mfano wa kuigwa kupitia tabia, mienendo na maamuzi yao ya kila siku.
Aidha amezitaka taasisi kuhakikisha kila mtumishi anapatiwa nakala ya kielektroniki ya Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma, kujengewa uwezo wa kuzizingatia na kutumia Hati ya Ahadi ya Uadilifu kama nyenzo ya kuimarisha uwajibikaji.
Amesema taasisi zinapaswa kufanya tathmini na tafiti za mara kwa mara ili kubaini kiwango cha uadilifu, maeneo yenye changamoto na kuchukua hatua stahiki kabla ukiukaji wa maadili haujaathiri utendaji wa taasisi.
Akizungumzia umuhimu wa kikao hicho, Kwarai alisema ushirikiano kati ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma ni muhimu katika kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usikivu wa watumishi wa umma.
Amesema kikao hicho kinatoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokabili usimamizi wa maadili katika sekta mbalimbali.
Amebainisha kuwa vikao hivyo vilianza mwaka 2018 kwa uratibu wa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, huku uandaaji wake ukifanyika kwa utaratibu wa kupokezana miongoni mwa taasisi shiriki.
Katika hatua ingine mezipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAO) kwa kuandaa vikao vya tano na sita vilivyofanyika Dodoma, huku Tume ya Utumishi wa Umma ikitarajiwa kuratibu kikao cha nane.
Amesema ushirikiano huo unapaswa kuendelezwa kwa kuzingatia maazimio yanayofikiwa na kuhakikisha kila taasisi inayopangiwa kuratibu kikao inaweka kipaumbele katika maandalizi yake.
Amesema kuanzia Julai 26, taifa limeanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, hivyo watumishi wa umma wanapaswa kutambua nafasi yao katika kufanikisha malengo hayo kwa kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Bi. Leila Mavika, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ,aliishukuru Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwa kuandaa kikao hicho na kusema mafunzo na uzoefu unaopatikana unapaswa kuwasilishwa katika taasisi zinazowakilishwa ili maazimio yaweze kutekelezwa kwa vitendo.
Amesema usimamizi wa maadili haupaswi kuishia katika majadiliano ya vikao pekee, bali unapaswa kuonekana katika mienendo ya watumishi na namna wanavyowahudumia wananchi.
Amesema washiriki watapata mawasilisho kutoka kwa wataalamu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Afya, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.
Ameeleza kuwa mada hizo zinalenga kuongeza uelewa kuhusu maadili katika sekta mbalimbali na kujenga uwezo wa taasisi katika kusimamia tabia na mienendo ya watumishi wa umma.





