NAHODHA WA NEW MV MWANZA KUSIMAMISHWA KAZI
Nov 26, 2026
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameiagiza Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (TASHICO) kumsimamisha kazi nahodha wa meli ya New MV Mwanza, Adam Mwisungu, baada ya uchunguzi kubaini kuwa ajali iliyotokea Novemba 18, mwaka huu katika Ziwa Victoria jijini Mwanza ilisababishwa na makosa ya kibinadamu.
Agizo hilo limekuja kufuatia uchunguzi wa tukio la meli hiyo kugonga mwamba wa Bismarck katika Bandari ya Mwanza Kaskazini wakati wa safari maalumu ya majaribio, huku Serikali ikieleza kuwa hakuna hitilafu ya kiufundi iliyobainika katika mifumo mikuu ya uendeshaji wa meli hiyo.
Akizungumza jijini Mwanza wakati akiwasilisha ripoti ya uchunguzi, Profesa Mbarawa amesema uchambuzi wa mazingira ya tukio na mahojiano yaliyofanyika kwa wahusika umeonesha kuwa meli ilikuwa katika hali nzuri ya kiufundi, lakini maamuzi yaliyofanywa wakati wa tukio hayakuwa sahihi.
Amesema teknolojia ya meli hiyo inahitaji wataalamu wenye uzoefu na uwezo wa kutambua mazingira hatarishi na kuchukua hatua zinazofaa kwa wakati, akisisitiza kuwa nafasi za uendeshaji haziwezi kukabidhiwa kwa watu wasiokuwa na umahiri unaotakiwa.
"Kama propela ingekuwa imepinda, meli ile isingeweza kusafiri kutoka Mwanza South kwenda Mwanza North Port. Uchunguzi haujabaini hitilafu yoyote ya kiufundi; kilichotokea ni makosa ya kibinadamu. Mtu hakufanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi," amesema.
Katika matokeo ya uchunguzi wa awali, Serikali imeeleza kuwa New MV Mwanza haikupata madhara makubwa yanayoathiri uimara wake, udhibiti wala mifumo yake mikuu ya uendeshaji, licha ya kupata mgongano katika sehemu ya mbele ya meli.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeielekeza TASHICO kufanya matengenezo ya sehemu ya mbele ya meli iliyoathiriwa na mgongano huo, chini ya usimamizi wa karibu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), sambamba na kukagua mifumo yote ya uendeshaji na usalama.
Aidha, Profesa Mbarawa ameitaka TASHICO kuchukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria dhidi ya nahodha, watumishi wengine na viongozi wenye dhamana ya usimamizi watakaobainika kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Amesisitiza kuwa Serikali haitaruhusu meli hiyo kuanza safari rasmi za kubeba abiria kabla ya kukamilika kwa matengenezo na ukaguzi unaohitajika, pamoja na kuhakikisha kuwa watumishi watakaopangiwa kuiendesha wana sifa na uzoefu wa kutosha.
"Tunahitaji watu ambao wana uwezo wa kukabiliana na mazingira yoyote yanayoweza kujitokeza wakati wa uendeshaji wa meli, hata kama ajali itatokea," amesema. Mbarawa.
Katika ajali hiyo iliyotokea wakati wa majaribio, hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa, huku pia kukiwa hakuna uchafuzi wa mazingira ulioripotiwa.
Profesa Mbarawa amewashukuru wananchi kwa utulivu waliouonesha wakati wa kusubiri matokeo ya uchunguzi na kuvitaka kupuuza taarifa zisizo rasmi zinazosambazwa mitandaoni, huku akivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi zilizoshiriki katika kushughulikia tukio hilo.



