Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MWIGULU AWATAKA WANAMICHEZO KUWA KIOO CHA MAADILI NA MALEZI BORA

MWIGULU AWATAKA WANAMICHEZO KUWA KIOO CHA MAADILI NA MALEZI BORA

 

Na Matukio Daima Media, Morogoro

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka wanamichezo nchini kutumia nafasi zao kuwa sauti ya jamii katika kupinga vitendo vya mmomonyoko wa maadili na kuwa mfano wa malezi bora, akisisitiza kuwa wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kujenga jamii yenye nidhamu na misingi imara ya kimaadili.



Dkt. Nchemba amesema hayo Novemba 12, 2026, mjini Morogoro wakati akifungua rasmi mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMUTA), akieleza kuwa vitendo vinavyodhoofisha maadili havipaswi kufumbiwa macho kwa kuwa vinaathiri ustawi wa nguvu kazi na maendeleo ya Taifa.

Amesema wanamichezo wana wajibu wa kuwa kioo cha jamii kwa kuonesha mwenendo unaozingatia maadili, huku akiwataka kuimarisha nidhamu ndani na nje ya viwanja vya michezo na kutambua kuwa kushinda na kushindwa ni sehemu ya ushindani wa kimichezo.

Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa uwazi na haki kwa waamuzi katika kusimamia michezo, akieleza kuwa uadilifu katika maamuzi ni msingi wa kuimarisha ushindani na kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza wakati wa mashindano.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nchemba amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mwanamichezo namba moja nchini, akitumia nafasi hiyo kuonesha umuhimu wa michezo katika kujenga umoja na kuitangaza Tanzania.


Ameeleza kuwa Tanzania inawakilishwa na timu nne katika mashindano ya Kombe la Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika, ambazo ni Simba SC, Yanga SC, Azam FC na Singida Black Stars.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amewahimiza Watanzania kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya michuano ya AFCON, akieleza kuwa tukio hilo kubwa la kimataifa ni fursa muhimu kwa nchi kuimarisha miundombinu, kuitangaza Tanzania na kukuza mshikamano wa kitaifa. Amesisitiza umuhimu wa kujenga hamasa, umoja, uzalendo na mshikamano miongoni mwa wananchi ili kuhakikisha Taifa linakuwa sehemu ya mafanikio ya kihistoria ya michuano hiyo.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, amesema mashindano hayo yana mchango chanya katika kukuza uchumi wa wananchi wa mkoa huo kupitia shughuli mbalimbali za kibiashara zinazochochewa na ujio wa washiriki na wageni wanaohudhuria mashindano hayo.

Naye Mwenyekiti wa SHIMUTA, Marcel Bituro,amesema mashindano ya SHIMUTA mwaka huu yamewakutanisha washiriki 4,500 kutoka taasisi 96, watakaoshindana katika michezo mbalimbali.

Waziri Mkuu pia ameshuhudia mchezo wa kuvuta kamba kwa timu za wanaume na wanawake, ambapo Bandari ya wanaume imeibuka mshindi dhidi ya PSSSF na kuendeleza rekodi yake ya kutetea ubingwa kwa miaka saba mfululizo.


Kwa upande wa wanawake, Mzinga imeibuka mshindi dhidi ya NBS na kuendelea kutetea ubingwa wake.


Mashindano hayo yameanza rasmi Novemba 12 na yanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 22, 2026 yakitumia viwanja mbalimbali vya michezo mjini Morogoro, ikiwemo uwanja wa Jamhuri, Mzinga, SUA na Bwalo  la JKT yakilenga kuimarisha afya, mshikamano, ushirikiano na ushindani wa kimichezo miongoni mwa watumishi na wadau kutoka sekta mbalimbali.


Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3