Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 DC SHAKA AITAKA KILOSA KUONGEZA UKUSANYAJI WA MAPATO

DC SHAKA AITAKA KILOSA KUONGEZA UKUSANYAJI WA MAPATO



- Asema Halmashauri ina uwezo wa kukusanya Sh bilioni 10 badala ya bilioni 8.4 zilizokadiriwa

- Wananchi wahimiza uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa vyanzo vya mapato

-

Na Matukio Daima Media, Kilosa

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka madiwani, viongozi wa kata na vijiji pamoja na watendaji wa Halmashauri hiyo kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato na kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma ili kuongeza uwezo wa Halmashauri kugharamia miradi ya maendeleo.

Shaka ametoa msisitizo huo wakati wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa lililofanyika katika Ukumbi wa FDC, likilenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema pamoja na Halmashauri hiyo kukadiria kukusanya Sh bilioni 8.4 katika mwaka wa fedha 2026/2027, tathmini ya vyanzo vilivyopo inaonesha kuwa ina uwezo wa kufikia hadi Sh bilioni 10 endapo kutakuwa na usimamizi madhubuti na uwajibikaji wa viongozi na watendaji.

Amesisitiza kuwa kila chanzo cha mapato kinapaswa kufanyiwa tathmini ili kubaini sababu za kutokusanya au kutofikia malengo, huku vinavyofanya vizuri vikiimarishwa zaidi, akieleza kuwa ni bora kuwa na vyanzo vichache vinavyokusanya kwa uhakika kuliko kuwa na vingi visivyozalisha mapato.

Aidha, amewataka viongozi wa kata na vijiji kutumia kamati za maendeleo kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake bila kusubiri maelekezo au ufuatiliaji kutoka kwa Mkuu wa Wilaya.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi Agnes John na Kipako Hakim wamehimiza viongozi na watendaji kuwajibika katika usimamizi wa mapato ya Halmashauri, wakieleza kuwa usimamizi mzuri utaongeza mapato yanayokusanywa na kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kwa nyakati tofauti wamesema uwajibikaji katika ukusanyaji na matumizi ya mapato utasaidia kuongeza uwezo wa Halmashauri hiyo kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo huduma za kijamii kama elimu, afya, maji na miundombinu, kupunguza upotevu wa fedha za umma na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Shaka amewahakikishia madiwani wa halmashauri hiyo kuwa maandalizi ya uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Pili wa mwaka 2026–2029 wa kukabiliana na kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji yanaendelea vizuri, akieleza kuwa mpango huo unalenga kuweka suluhisho la kudumu la changamoto hiyo wilayani humo.


Amesema mpango huo umejengwa katika nguzo tano, huku akiwataka viongozi na wananchi kushirikiana katika utekelezaji wake na kuendelea kuwa mabalozi wa amani ili kulinda usalama na kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea.

Ameongeza kuwa uwajibikaji, ushirikiano na misingi ya utawala bora ni mambo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu na kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha maisha ya wananchi.

Mwisho



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3