Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WADHIBITI UBORA WATAKIWA KUSIMAMIA USALAMA WA WANAFUNZI

WADHIBITI UBORA WATAKIWA KUSIMAMIA USALAMA WA WANAFUNZI

Wathibiti ubora wa shule nchini wametakiwa kutumia maarifa waliyoyapata katika mafunzo ya Shule Salama kuimarisha usimamizi wa mazingira ya kujifunzia, lishe, afya na ustawi wa wanafunzi ili shule ziwe sehemu salama kwa watoto.

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Grace Mbilinyi, wakati akifunga mafunzo ya siku nne kwa maafisa hao yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza.

Mbilinyi amesema mafunzo hayo yamewajengea washiriki uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, hivyo wanapaswa kuhakikisha elimu waliyoipata inatumika kuboresha hali halisi ya shule wanazozisimamia.

Amesema wathibiti ubora wana nafasi muhimu katika kuhakikisha changamoto zinazoweza kuhatarisha usalama na maendeleo ya watoto zinabainishwa na kutafutiwa ufumbuzi kwa wakati.

Amewataka kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhusu usalama wa wanafunzi, ikiwamo kufungwa kwa shule kwa mujibu wa kalenda na maelekezo rasmi yaliyotolewa kutokana na tahadhari za hali ya hewa.

Awali, Mratibu wa Mafunzo katika Kituo cha Mwanza, Majaliwa Mkalawa, amesema katika vituo walivyoratibu walifanikiwa kuwafikia maafisa uthibiti ubora 703 kati ya 722 waliolengwa kutoka mikoa 13.

Amesema kati ya waliofikiwa, wanaume ni 438 na wanawake 265, huku lengo la mafunzo hayo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kufanya tathmini za shule na kutoa ushauri unaoweza kuboresha mazingira ya utoaji elimu.



Mkalawa amesema mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), huku mkakati ukiwa ni kuhakikisha programu hiyo inaendelea hata baada ya mradi kumalizika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Butimba Nicholaus Magige, ameipongeza wizara kwa kutumia chuo hicho kuendesha mafunzo hayo na kuwataka wathibiti ubora kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kutenganisha mahusiano binafsi na wajibu wa kikazi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usimamizi wa ubora wa elimu na kuhakikisha mazingira ya shule yanazingatia mahitaji ya msingi ya usalama na ustawi wa wanafunzi.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3