Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 KIHONGOSI AAGIZA BARABARA MOJA IRINGA MJINI KUPEWA JINA LA EDDO MNYAMA ILI KUMUENZI.

KIHONGOSI AAGIZA BARABARA MOJA IRINGA MJINI KUPEWA JINA LA EDDO MNYAMA ILI KUMUENZI.

MATUKIO DAIMA MEDIA.

IRINGA.Katibu wa Itikadi, Mafunzo na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Iringa kutafuta barabara moja ndani ya Manispaa ya Iringa na kuipa jina la marehemu Eddo Bashiri, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi na kutambua mchango wake katika jamii.

Akizungumza wakati wa shughuli ya kumuaga marehemu iliyofanyika katika viwanja vya KKKT Kibwawa, Kihongosi amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mchango wa Eddo Bashiri unaendelea kukumbukwa, hususan katika kuibua na kukuza vipaji vya vijana wa Iringa.

“Marehemu alikuwa na mchango mkubwa katika kuwainua vijana, kuwaunga mkono na kupambania vipaji vyao, hivyo ni muhimu juhudi zake kutambuliwa na kuendelezwa hata baada ya kifo chake”alisema Kihongosi

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Iringa Mjini Fadhili Ngajilo amewashukuru wananchi wa Iringa kwa kujitokeza kwa wingi kutoa pole na kuungana na familia ya marehemu Edwin Bashiri, huku akitangaza maandalizi ya shughuli maalumu ya kumuenzi marehemu siku ya arobaini tangu kufariki kwake.

Ngajilo  alisema marehemu Edwin Bashiri alikuwa mtu aliyefahamika na kupendwa na watu wengi kutokana na mchango wake katika jamii, hivyo kuna umuhimu wa kuendeleza mazuri aliyoyaacha.

“Heshima na mchango wa marehemu vinapaswa kuhifadhiwa kwa vitendo, akiwataka viongozi na madiwani kushirikiana kuweka kumbukumbu ya kazi kubwa alizozifanya, ikiwemo pendekezo la kutenga mchango maalumu wa kumuenzi katika majengo yao”

Aidha,  amewaagiza viongozi na maafisa wa ofisi yake ya ubunge kuanza maandalizi ya shughuli maalumu ya kumbukumbu itakayofanyika siku ya arobaini, ambayo itakuwa katika mfumo wa tamasha litakalowakutanisha wananchi mbalimbali kwa ajili ya kumkumbuka marehemu.

Alisisitiza kuwa ingawa maisha ya Edwin Bashiri yamehitimishwa, mchango na matendo yake mema yanapaswa kuendelea kuwa sehemu ya historia ya jamii ya Iringa.

MWISHO




Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3