Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
JUMUIYA YA WAZAZI CCM KUTOWAVUMILIA WANAOKWENDA KINYUME NA MSIMAMO WA CHAMA

JUMUIYA YA WAZAZI CCM KUTOWAVUMILIA WANAOKWENDA KINYUME NA MSIMAMO WA CHAMA

 



Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media DODOMA


JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetangaza kuendelea kusimama imara katika kulinda misingi na maslahi ya chama hicho, ikieleza kuwa haitawavumilia watu wanaokwenda kinyume na msimamo wake.


Mwenyekiti wa Taifa wa jumuiya hiyo, Fadhili Maganya, amesema wataendelea kutumia nafasi zao kukitetea chama na kueleza misimamo yake, huku wakidumisha uungwaji mkono kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.


Alitoa msimamo huo November 27,2026 jijini hapa wakati wa kufungua mafunzo ya watendaji wa jumuiya hiyo, yaliyowakutanisha makatibu wa mikoa na wilaya kwa lengo la kuwaimarisha katika usimamizi na utekelezaji wa majukumu yao.


Maganya amesema wakati CCM ikijiandaa kuelekea uchaguzi mwakani, ni muhimu kwa watendaji wa jumuiya hiyo kuwa na msimamo mmoja katika kutetea chama na kuhakikisha ujumbe wake unawafikia wananchi.



Ameeleza kuwa Jumuiya ya Wazazi ina wajibu wa kuwa sehemu ya juhudi za kukijenga na kukisemea chama, akiwataka watendaji kutotishwa na watu wanaopinga misimamo ya CCM.


“Chama hiki bado imara, muendelee kukisemea pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan. Jumuiya ya Wazazi itatumika kama kipaza sauti cha kukisemea chama na hatutakuwa na woga wowote kwa mtu anayekwenda kinyume na Chama Cha Mapinduzi,” amesema.


Katika kuonyesha msimamo wa jumuiya hiyo kuhusu uongozi wa Rais Samia, Maganya amesema wataendelea kumuunga mkono na kumpongeza hadi atakapofikia uamuzi wa kuhitimisha safari yake ya uongozi.


“Tutakuwa wa mwisho kumuaga na kumpongeza Rais mpaka pale atakaposema anataka kwenda kupumzika kwake Kizimkazi,” amesema.


Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Ali Hapi, amesema mabadiliko ya kiutendaji na kijamii yanahitaji watendaji kuwa na uelewa mpya ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.



Amesema katika kipindi cha miaka 12 iliyopita kumekuwa na mabadiliko makubwa yanayogusa namna taasisi na viongozi wanavyotekeleza majukumu yao, hivyo mafunzo endelevu ni muhimu katika kuwajengea uwezo wa kukabiliana na mazingira hayo.


Amebainisha kuwa kukua kwa matumizi ya mitandao ya kijamii ni mojawapo ya mabadiliko yanayopaswa kuzingatiwa na watendaji, akiwataka kuongeza ubunifu na nidhamu katika matumizi ya njia mbalimbali za mawasiliano.


Hapi amesema mafunzo hayo yameandaliwa pia kuwajengea washiriki uelewa kuhusu maadili na mipaka ya uongozi, usimamizi wa muda, mawasiliano bora, mahusiano ya kikazi na mbinu za kuandaa taarifa zinazokidhi mahitaji ya kiutendaji.


“Tunawaomba muwe tayari kujifunza. Hii ni nafasi ya kujifunza kutoka kwa wenzenu waliofanya vizuri na kutumia uzoefu huo kuboresha maeneo ambayo hatujafanya vizuri,” amesema.


Amesema watendaji wanapaswa kujitathmini katika namna wanavyotekeleza majukumu yao, ikiwamo kuzingatia muda wa kazi, kutumia lugha inayofaa na kuwa na mwenendo unaowezesha kujenga mahusiano mazuri na watu wanaowazunguka.


Ameongeza kuwa uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja na jumuiya nyingine ndani ya CCM ni eneo jingine linalohitaji kuimarishwa ili kuongeza ufanisi katika shughuli za chama.


Aidha, amesema ubora wa taarifa zinazotolewa na watendaji ni sehemu muhimu ya uwajibikaji, hivyo wanapaswa kuzingatia kanuni za uandishi na uwasilishaji wa taarifa ili kurahisisha mawasiliano na tathmini ya utekelezaji wa majukumu.


Hapi amewataka washiriki kutokuchukulia mafunzo hayo kama tukio la kawaida, bali wayatumie kujipima, kujifunza kutoka kwa wenzao na kupata majibu ya changamoto zinazojitokeza katika utendaji wao wa kila siku



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3