Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MAONESHO YA MADINI YAIPAISHA LINDI KIMAPATO - MAKUSANYO YAFIKIA BILIONI 10.5

MAONESHO YA MADINI YAIPAISHA LINDI KIMAPATO - MAKUSANYO YAFIKIA BILIONI 10.5



Na Hadija omary 

LINDI.....Mkoa wa Lindi umeandikisha mafanikio makubwa katika Sekta ya Madini baada ya makusanyo ya maduhuli ya Serikali kuongezeka kwa zaidi ya mara nne ndani ya kipindi cha miaka sita.

Hayo yamebainishwa na Afisa Madini Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emmanuel Shija, alipozungumza kuhusu mwenendo wa sekta hiyo na maandalizi ya Maonesho Makubwa ya Kimataifa ya Madini yanayotarajiwa kufanyika Wilayani Ruangwa.

Mhandisi Shija amesema kuwa kwa miaka sita iliyopita, Mkoa wa Lindi ulikuwa unakusanya maduhuli ya wastani wa Shilingi Bilioni 2.5 pekee, lakini katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, makusanyo hayo yamepanda hadi kufikia takribani Bilioni 10.5.

"Mkoa wetu wa Lindi ulikuwa unakusanya maduhuli ya Serikali Bilioni 2.5 lakini mpaka kufika mwaka uliopita wa fedha Mkoa wetu wa Lindi umeweza kukusanya Bilioni takribani 10.5," amesema Mhandisi Shija.

Ameeleza kuwa ongezeko hilo linatokana na ukuaji mkubwa wa sekta ya madini mkoani humo na mikakati madhubuti iliyowekwa na Serikali ya Mkoa, ikiwemo kuanzishwa kwa Soko la Madini na Maonesho ya Madini yanayofanyika kila mwaka.

Kwa mujibu wa Mhandisi Shija, ukuaji huo unaonekana pia katika biashara ya dhahabu. Amesema mwaka 2020/2021 Mkoa ulifanya biashara ya dhahabu ya takribani kilogramu 100 tu, wakati mwaka wa fedha wa 2025/2026 kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia kilogramu 240 zilizopita katika Soko la Madini lililopo Wilayani Ruangwa.

Aidha, ametoa wito kwa wadau wa madini wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kuchangamkia fursa kubwa za uwekezaji zilizopo Mkoani Lindi.

Amesema fursa hizo zinatangazwa zaidi kupitia Maonesho Makubwa ya Kimataifa ya Madini na Fursa za Uwekezaji yanayotarajiwa kufanyika kuanzia *tarehe 16 hadi 19, 2026, Wilayani Ruangwa.*

Maonesho hayo ambayo yanatarajiwa kushirikisha wadau kuanzia ngazi ya chini, kitaifa na kimataifa na yamebeba Kauli Mbiu isemayo "Madini na Teknolojia, Fursa ya Kiuchumi Lindi".

Mwisho




 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3