Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
GEITA KUPATA MSUKUMO MPYA WA UWEKEZAJI KUPITIA UMEME

GEITA KUPATA MSUKUMO MPYA WA UWEKEZAJI KUPITIA UMEME


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

SHUGHULI za uzalishaji na uwekezaji mkoani Geita zinatarajiwa kupata msukumo mpya baada ya Serikali kuanza utekelezaji wa mradi wa Sh bilioni 63.19 wa kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka Mpomvu hadi kituo cha GGM.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 220 yenye urefu wa kilomita 6.7, huku ukilenga kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme linalotokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo hilo.

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha miundombinu ya nishati inaendana na kasi ya ukuaji wa uchumi na mahitaji ya wananchi pamoja na wawekezaji.

Amesema uwekezaji katika miundombinu hiyo unatarajiwa kuongeza uhakika wa umeme na kutoa mazingira bora kwa shughuli za uzalishaji, jambo litakaloweza kuongeza ajira, mapato na kuvutia uwekezaji zaidi mkoani humo.

“Tunataka kuona umeme unaozalishwa nchini ukitumika kikamilifu kuchochea uzalishaji, kuongeza ajira, kuongeza mapato na kuvutia uwekezaji zaidi miradi huu ni kielelezo cha falsafa hiyo,” alisema Makamba.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema utekelezaji wa mradi huo utachukua miezi 18 kuanzia siku ya kusainiwa kwa mkataba, akibainisha kuwa moja ya malengo yake ni kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya umeme kwa GGM.

Amesema GGM ni miongoni mwa wateja wakubwa wa TANESCO wanaochangia mapato makubwa kwa Shirika, hivyo kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na manufaa kwa TANESCO, mteja huyo na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Balozi Zuhura Bundala, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uwezo wa Shirika kuhudumia mahitaji ya wateja na wakati huo huo kuweka msingi wa fursa mpya za uwekezaji na ajira.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, amesema hatua hiyo inaonyesha namna sekta ya nishati na madini zinavyoweza kushirikiana katika kuimarisha uchumi wa kisasa unaolenga kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashimu Komba, ameyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, alisema Serikali ya mkoa iko tayari kushirikiana na mkandarasi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa bila vikwazo na kukamilika kwa wakati.

Amesema kukamilika kwa njia hiyo mpya kutasaidia kuachia njia ya awali ya msongo wa kilovoti 33 kuendelea kunufaisha wananchi wa Geita na maeneo ya jirani, huku mfumo mpya ukiongeza uwezo wa kusafirisha umeme na kuwezesha shughuli za uzalishaji na uwekezaji kuendelea kukua.







 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3