WAZIRI WA FEDHA AVUTIWA NA TEKNOLOJIA YA UFUGAJI WA SAMAKI
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima MediaDodoma
WAZIRI wa Fedha, Khamis Mussa Omary, amesema matumizi ya teknolojia za kidijitali katika ufugaji wa samaki ni miongoni mwa njia zitakazoongeza uzalishaji, kufungua fursa za kiuchumi na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la sekta ya uvuvi katika Maonesho ya 88 ya Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Samweli Malechela, mkoani Dodoma, Omary amesema ubunifu unaotumika katika uzalishaji wa samaki unaonyesha namna teknolojia inavyoweza kuleta mapinduzi katika sekta za uzalishaji.
Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali yamepanua fursa za uzalishaji wa samaki, kuongeza tija na kupunguza utegemezi wa uvuvi wa asili, hatua inayochangia kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi.
Mbali na hilo, Waziri Omary aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kuimarisha huduma za ugani kupitia kuwawezesha maafisa ugani vitendea kazi, ikiwemo usafiri, jambo linalowarahisishia kuwafikia wakulima na kuwapatia huduma kwa wakati.
Amesema juhudi hizo zinaongeza ufanisi wa huduma za ugani, kuimarisha uzalishaji wa mazao na kuwawezesha wakulima kutumia mbinu bora za kilimo.
Waziri huyo pia amezitaka taasisi za uzalishaji nchini kuimarisha ushirikiano katika kutatua changamoto zinazozikabili ili kuongeza tija na kuharakisha maendeleo ya sekta mbalimbali.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa taasisi, matumizi ya teknolojia na uwekezaji katika huduma za ugani ni msingi muhimu katika kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.



