Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
POLISI KATA AJITOKEZA KUMSAIDIA MJANE ALIYEUNGULIWA NYUMBA NA MOTO

POLISI KATA AJITOKEZA KUMSAIDIA MJANE ALIYEUNGULIWA NYUMBA NA MOTO

Na Matukio Daima Media, Morogoro

MAMA mjane wa watoto wanne, Hadija Yahaya Mohamed (30), mkazi wa Kitongoji cha Tongoma A, Kijiji cha Mbwade, Kata ya Bwakila Chini, Wilaya ya Morogoro, anaendelea kukabiliwa na hali ngumu ya maisha baada ya nyumba yake kuteketea kwa moto na kumwacha yeye pamoja na watoto wake bila makazi ya kudumu.


Hadija anasema tukio hilo linamrudisha kwenye maumivu aliyowahi kuyapitia hapo awali, kwani hii ni mara ya pili nyumba yake inateketea kwa moto.

Anasema siku ya tukio anatoka nyumbani baada ya kumaliza kufanya usafi na kwenda kununua sabuni pamoja na vitafunwa, lakini anaporejea anakuta nyumba yake ikiungua moto huku wananchi wakijitahidi kuokoa mali zilizokuwa ndani.

Kutokana na hali yake ya kiuchumi, Hadija anasema hana uwezo wa haraka wa kujenga nyumba nyingine, hali inayomlazimu yeye na watoto wake kuomba hifadhi kwa majirani.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tongoma A, Peter Mwimbila, anasema tukio hilo limeiweka familia hiyo katika mazingira magumu na kwamba inahitaji msaada wa jamii ili iweze kupata makazi ya kudumu.

Hata hivyo, katika wakati ambao familia hiyo inakabiliwa na changamoto hiyo, msaada umeanza kupatikana baada ya Polisi Kata wa Bwakila Chini, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Flora Mwandi, kutoa vifaa vya ujenzi na mahitaji mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili

Msaada huo unahusisha matofali, mifuko ya saruji, bati na misumari kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba, pamoja na vyombo na chakula kwa ajili ya familia hiyo.


Mkaguzi Mwandi anasema ameamua kutoa msaada huo baada ya kuguswa na hali ya mama huyo na watoto wake, ambao kwa sasa hawana makazi ya kudumu.



Katibu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF Net) Mkoa wa Morogoro, Inspekta Zuwena Mwita, anasema hatua hiyo inaonyesha umuhimu wa Polisi kuwa karibu na jamii na kutambua changamoto zinazowakabili wananchi.


Kwa sasa, msaada huo unatoa matumaini kwa Hadija na watoto wake kuanza safari ya kujenga upya maisha yao, huku familia hiyo ikihitaji msaada zaidi ili iweze kurejea katika makazi yake.


Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3