WANAFUNZI ST DOMINIC SAVIO WAFURAHIA ZIARA YA KIMASOMO NCHINI KENYA
NA MATUKIO DAIMA MEDIA KENYA
Jumla ya wanafunzi Zaidi ya 80 wa Shule za St. Dominic Savio Kigonzile na Cagliero wameanza ziara ya mafunzo kwa vitendo nchini Kenya ikiwa ni sehemu ya programu ya kuwajengea uwezo wa kujifunza nje ya mazingira ya darasani.
Akizungumzia ziara hiyo Mratibu wa shule hizo Mussa Myula alisema lengo kuu la ziara hiyo ni kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo kupitia maeneo mbalimbali watakayoyatembelea nchini Kenya.
Alisema wanafunzi watapata fursa ya kujifunza kuhusu jiografia, miundombinu ya barabara, vivutio vya utalii, tamaduni na maisha ya wananchi wa nchi jirani, jambo litakalowasaidia kupanua upeo wa maarifa na uelewa wao kuhusu Afrika Mashariki.
Myula alieleza kuwa pamoja na kuona mambo mazuri yanayofanywa nchini Kenya, wanafunzi watajifunza namna yanavyoweza kuwa chachu ya maendeleo kwa jamii yao.
“Ziara za mafunzo ni sehemu ya utamaduni wa Shule za St. Dominic Savio na Kariello, ambapo kila mwaka wanafunzi hupata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania ili kuongeza maarifa na uzoefu wa maisha”
Aliongeza kuwa kabla ya safari hiyo ya Kenya, wanafunzi wa shule hizo walishiriki ziara Bungeni jijini Dodoma na kujifunza masuala ya bunge, na shughuli za maendeleo, jambo ambalo lilizaa matokeo chanya kwa wanafunzi hao waliporejea shuleni.
“Baada ya kumaliza ziara ya Kenya, wanafunzi wanatarajiwa kuendelea na ziara nyingine ya mafunzo visiwani Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya ratiba ya shule ya kuwapa wanafunzi uzoefu mpana zaidi wa mazingira tofauti”
Kwa upande wake, mmoja wa mwanafunzi wanaoshiriki katika ziara hiyo alisema ziara hizo zinawapa wanafunzi fursa ya kujifunza mambo mapya ambayo hayawezi kupatikana darasani pekee, huku akiwahimiza wazazi kuzingatia shule zinazowapa watoto nafasi ya kushiriki mafunzo ya vitendo.TAZAMA SHANGWE YA WANAFUNZI WAKIWA KENYA BOFYA LINK HII
“Natarajia kujifunza mambo mbalimbali nchini Kenya ikiwemo utamaduni, vivutio na mazingira ya nchi hiyo, uzoefu wa nchini Kenya utamsaidia kuongeza maarifa na kujiamini zaidi”
Aidha, ziara za aina hiyo huchangia kuwajengea wanafunzi kujiamini, kuwapanua mtazamo wa maisha na kuwapa hamasa ya kujifunza kutoka kwa mataifa mengine, huku wakihifadhi maadili na uzalendo kwa nchi yao.





