Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DIB: KIWANGO CHA FIDIA YA AMANA CHAFIKIA SH. MILIONI 7.5

DIB: KIWANGO CHA FIDIA YA AMANA CHAFIKIA SH. MILIONI 7.5

 

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma

BODI ya Bima ya Amana (DIB) imesema kiwango cha juu cha fidia kwa mteja mwenye amana katika benki au taasisi ya fedha inayofungwa au kufilisika kwa sasa ni Sh milioni 7.5, huku ikiwahimiza wananchi wenye madai ambayo bado hawajayawasilisha kujitokeza ili waweze kulipwa stahiki zao.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 88 ya Nanenane yanayoendelea Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa DIB, Isack Nikodem, alisema kiwango hicho kimewekwa kwa mujibu wa sheria inayosimamia kinga ya amana nchini.

Amesema wateja waliokwisha kulipwa asilimia 85 ya fidia katika awamu ya kwanza hawapaswi kuwa na wasiwasi, kwani taarifa zao tayari zipo katika mfumo wa DIB na kiasi kilichobaki kitaingizwa moja kwa moja kwenye akaunti zao baada ya taratibu kukamilika.

Nikodem amesema bado kuna wateja 428 ambao hawajajitokeza kuwasilisha madai yao, hivyo akawataka kutumia fursa hiyo ili waweze kunufaika na kinga ya amana inayotolewa na taasisi hiyo.

Amefafanua kuwa DIB ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kulinda amana za wananchi walioweka fedha katika benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kuhakikisha wanapatiwa fidia pale taasisi hizo zinaposhindwa kuendelea na shughuli zake.


Aidha, amesema fedha zinazotumika kulipa fidia zinatokana na michango inayochangwa na benki zote na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania, kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa katika sheria.

Nikodem amesema mfumo wa kinga ya amana umeanzishwa ili kuongeza imani ya wananchi katika sekta ya fedha na kuhakikisha waweka amana hawapotezi fedha zao wanapojitokeza changamoto zinazosababisha benki au taasisi za fedha kufungwa.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3