Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 WAZIRI MKUU AITAKA TADB KUPANUA UWEZO WA KUFADHILI WAKULIMA

WAZIRI MKUU AITAKA TADB KUPANUA UWEZO WA KUFADHILI WAKULIMA


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

WAZIRI Mkuu ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuongeza uwezo wake wa kifedha na kupanua wigo wa utoaji wa mikopo ili kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuharakisha mageuzi ya sekta ya kilimo na kuimarisha uchumi wa nchi.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma, amesema benki hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya Serikali katika kuwezesha uwekezaji kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kupitia utoaji wa mitaji kwa wazalishaji na wawekezaji mbalimbali.

Amesema ili Tanzania ifikie malengo ya kuongeza uzalishaji wa mazao na kuhakikisha usalama wa chakula, kuna haja ya kuendelea kuiwezesha TADB kifedha ili iweze kujibu mahitaji makubwa ya wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo.


Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali haiwezi kutegemea ruzuku pekee kila mwaka katika kuendeleza sekta ya kilimo, hivyo taasisi za kifedha kama TADB zina jukumu kubwa la kuhakikisha mitaji inapatikana kwa wakati kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.

Amesisitiza kuwa benki hiyo inapaswa kuongeza uwezo wa kufadhili ununuzi wa mbolea, pembejeo, zana za kisasa za kilimo pamoja na miradi ya kuongeza thamani ya mazao ili kuongeza tija na ushindani wa bidhaa za Tanzania.

Aidha, ameitaka TADB kushirikiana kwa karibu na Wizara za Kilimo na Mifugo pamoja na TAMISEMI katika kuwekeza kwenye miundombinu ya baada ya mavuno, hususan ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao, hatua itakayosaidia kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa kutumia mazao yao kama dhamana.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji  wa TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imeendelea kufadhili miradi mbalimbali ya kimkakati inayochochea ukuaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi nchini.


Amesema zaidi ya shilingi bilioni 700 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji, huku zao la kahawa kutoka mikoa ya Kagera na Kigoma kupitia vyama vya ushirika likiwa miongoni mwa mafanikio yaliyowavutia wadau wengi waliotembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane.


Nyabundege amesema TADB pia imewezesha mradi wa kisasa wa ufugaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo, unaotumia teknolojia kutoka Misri na wenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 90 za samaki kwa mwezi, huku ukizingatia uhifadhi wa mazingira na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo umechangia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo na uvuvi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mwisho



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3