Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
BRELA YABORESHA MFUMO WA USAJILI, YASOGEZA HUDUMA MAONESHO YA NANE NANE

BRELA YABORESHA MFUMO WA USAJILI, YASOGEZA HUDUMA MAONESHO YA NANE NANE

 

N


a Hamida Ramadhan, Matukio Media, Dodoma

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umebainisha kuwa umefanya maboresho makubwa katika mfumo wake wa usajili ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, sambamba na kusogeza huduma hizo katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nane Nane, Dodoma, kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti Nane mwaka huu.


BRELA imesema wananchi wanaotembelea maonesho hayo wanapata huduma mbalimbali za usajili na leseni ambazo kwa kawaida huzipata katika ofisi za taasisi hiyo, huku pia wakipewa elimu kuhusu maboresho ya mfumo mpya wa usajili ulioboreshwa.


Waziri Mkuu pia alitembelea banda la BRELA katika Maonesho ya Nane Nane, ambapo alijionea namna taasisi hiyo inavyoendelea kutoa huduma kwa wananchi na wafanyabiashara, pamoja na kupata maelezo kuhusu maboresho ya mfumo wa usajili unaorahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali.


Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Usajili wa BRELA, Yusuf Mwasakafika, amesema wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, utoaji wa leseni za biashara Kundi A pamoja na huduma zinazohusiana na usajili wa alama za biashara na viwanda.


Amesema uwepo wa BRELA katika maonesho hayo unalenga pia kuwahamasisha wakulima wanaofanya kilimo cha kibiashara kurasimisha shughuli zao ili waweze kujiamini zaidi katika kufanya biashara na kufikia masoko na wadau mbalimbali.


“Tunawahamasisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanaofanya shughuli mbalimbali za kilimo kufika hapa na kupata huduma ambazo wangeweza kuzitafuta wakiwa ofisini, lakini sasa wanaweza kuzipata hapa,” amesema Mwasakafika.


Aidha, amesema BRELA inatumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu mfumo mpya wa usajili ulioboreshwa, ambao umefanyiwa maboresho ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza changamoto ambazo baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakikumbana nazo.


Kwa mujibu wa Mwasakafika, kupitia mfumo huo mpya, baadhi ya huduma zinaweza kufanyika kwa njia ya mtandao bila mhusika kulazimika kufika moja kwa moja katika ofisi za BRELA.


Amesema miongoni mwa maboresho yaliyofanyika ni kuwezesha uwasilishaji wa nyaraka mbalimbali kwa njia ya mfumo, ikiwemo nyaraka zinazohusiana na madeni yanayohitaji kuwasilishwa katika usajili.


“Kwa kutumia mfumo huu sasa tumeweza kuboresha huduma kiasi kwamba mtu anaweza kuwasilisha nyaraka akiwa nyumbani kwake au benki, bila kulazimika kufika BRELA,” amesema.


Amesema pia mfumo huo umeboresha upatikanaji wa taarifa za kampuni kwa wananchi wanaohitaji taarifa hizo, huku ukiongeza uwazi wa taarifa za kampuni kulingana na huduma inayohitajika.


Mwasakafika amesema maboresho mengine ni katika suala la usalama wa taarifa za kampuni, ambapo wanahisa hupata taarifa pale kampuni inapofanya mabadiliko yanayohusiana na kampuni zao.


Hata hivyo, amewataka wananchi wanaotaka kutumia mfumo huo kuhakikisha wanakuwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), namba ya simu inayotumika pamoja na anuani sahihi ya barua pepe, ambazo ni muhimu katika kupata huduma kupitia mfumo.


BRELA inasimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali zinazohusu usajili na urasimishaji wa biashara nchini, ikiwemo usajili wa kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma za leseni zinazohusika na taasisi hiyo.


Katika Maonesho ya Nane Nane, BRELA inapatikana katika banda la Makamu wa Rais na Waziri Mkuu pamoja na banda la Wizara ya Viwanda na Biashara, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi na kuwapatia huduma pamoja na elimu kuhusu urasimishaji wa shughuli zao za biashara.


Mwisho



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3