Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAKULIMA WAHAMASISHWA KUTUMIA KILIMO IKOLOJIA HAI

WAKULIMA WAHAMASISHWA KUTUMIA KILIMO IKOLOJIA HAI

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

WAKULIMA nchini wametakiwa kuhamia katika matumizi ya pembejeo za kilimo ikolojia hai ili kulinda afya za walaji, kuhifadhi mazingira na kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao, huku matumizi holela ya kemikali yakitajwa kuongeza hatari ya magonjwa na kuharibu rutuba ya udongo.


Wito huo umetolewa na Mratibu wa Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO), Abdallah Mkindi, wakati wa mdahalo kuhusu pembejeo za kilimo ikolojia hai uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo kwenye Maonesho ya Nanenane, ulioandaliwa na TABIO, ambapo wadau wa sekta ya kilimo walijadili nafasi ya pembejeo za asili katika kuimarisha uzalishaji endelevu.


Mkindi amesema kilimo ikolojia hai kinatoa suluhisho la uzalishaji endelevu kwa kuwa kinazingatia afya ya binadamu, mazingira na uchumi wa mkulima. 


Amesema matumizi makubwa ya kemikali katika kilimo yameendelea kuzua hofu kutokana na tafiti mbalimbali kuonesha kuwa matumizi yasiyo sahihi yanaweza kuongeza hatari ya magonjwa mbalimbali, ikiwemo baadhi ya saratani, pamoja na uchafuzi wa udongo na vyanzo vya maji.

"Hii ndiyo sababu tunaendelea kuwajengea uwezo wakulima kutumia mbinu rafiki kwa mazingira tunataka mkulima azalishe chakula salama, alinde afya yake, familia yake na mlaji kwa ujumla huku akihifadhi rutuba ya ardhi kwa vizazi vijavyo," amesema.


Katika mdahalo huo, Mwija Irika kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania alisema Sheria ya Mbolea imefungua fursa mbalimbali kwa wawekezaji na wazalishaji wa mbolea za asili, huku taratibu za usajili zikiwa wazi na rafiki kwa wawekezaji.


Amesema hadi sasa zaidi ya aina 65 za mbolea za asili zimesajiliwa nchini, huku wazalishaji 15 tayari wakifanya shughuli za uzalishaji, jambo linaloonesha ukuaji wa sekta hiyo kutokana na Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uzalishaji na matumizi ya pembejeo za kilimo ikolojia hai.


"Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na tunashuhudia kampuni mbalimbali zikiingia katika uzalishaji wa mbolea za asili pia tunaendelea kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea hizo ili kuongeza tija na kulinda afya ya udongo," amesema.


Irika ameongeza kuwa matumizi ya mbolea za asili yana mchango mkubwa katika kuboresha rutuba ya udongo kwa muda mrefu, kupunguza gharama za uzalishaji na kuchangia uzalishaji wa mazao salama kwa walaji.


Naye Senior Program Coordinator wa CSWED Tanzania, Gladness Martini, alisema tafiti shirikishi zimekuwa na mchango mkubwa katika kuwasaidia wakulima kutambua, kuzalisha na kuhifadhi mbegu za asili zenye ubora.


Amesema kupitia ushirikishwaji wa wakulima katika hatua zote za utafiti, wanajengewa uwezo wa kuelewa nafasi yao katika maendeleo ya teknolojia za kilimo na kunufaika moja kwa moja na matokeo ya tafiti hizo.


Martini aliongeza kuwa mbegu za asili zinazofanyiwa utafiti na kuthibitishwa kisayansi zina uwezo wa kuongeza uzalishaji huku zikiendana na mazingira ya maeneo husika, hivyo kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wakulima.


Amewataka wadau wa maendeleo kuendelea kuwekeza katika tafiti na mafunzo kwa wakulima ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya wanufaika wa matokeo ya utafiti na kuchochea matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira katika sekta ya kilimo.


Kwa upande wake, mkulima mtafiti Julina David alisema pamoja na jitihada hizo bado wakulima wengi wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo za asili, hususan viuatilifu ambavyo havipatikani kwa urahisi kwenye maduka ya pembejeo.


Amesema ruzuku nyingi zimeendelea kuelekezwa kwenye pembejeo za viwandani, hali inayowafanya baadhi ya wakulima kukata tamaa ya kutumia mbinu za kilimo ikolojia hai.


"Tunahitaji mifumo bora kuanzia ngazi ya kaya ya kuwasaidia wananchi kujifunza namna ya kutengeneza mbolea na viuatilifu vya asili kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao  elimu ndiyo msingi wa mafanikio ya kilimo hiki," amesema.


Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo inayolinda mazingira katika uzalishaji wa mbolea za asili ili kuhakikisha teknolojia hizo zinakuwa endelevu na zenye manufaa kwa wakulima.


Naye mdau wa kilimo, Ismail Shaban, amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza elimu kwa wakulima kuhusu faida za mbolea za asili na namna ya kuzitumia kwa usahihi.


Amesema wakulima wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu uwezo wa pembejeo hizo kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama za kilimo, jambo linalochangia matumizi yake kuwa madogo.


Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3